Kinana: Viongozi igeni mfano wa Rais Samia

GEITA: MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amewataka viongozi na makada wa Chama hicho kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na Katiba wanapowakosoa watendaji hususani wateule wa Rais.

Amesema ni vyema wakajifunza kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye pamoja na kuwa na uwezo na mamlaka lakini hajawahi kusimama hadharani na kuvunja haki ya utu wa mtu hususani watendaji katika ngazi mbalimbali.

Kinana ameyasema hayo leo Desemba 13 katika uzinduzi wa ofisi za CCM wilayani Bukombe mkoani Geita.

Amesema, “nataka kufafanua hili ni kwamba viongozi wasimamie watendaji serikalini, wasimamie sheria, kanuni na utaratibu lakini si vizuri kuwasema hadharani na kuwafedhehesha watendaji wa serikali.

“Mfano mzuri wa kuigwa ni wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwani hatujawahi kuona akisimama hadharani akimfedhehesha mtendaji kwa sababu yeye ni muumini wa utawala bora, unaozingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu,” amesema.

Pia, amesema kuwa watendaji hao wanasimamiwa na tume mbalimbali zinazosimamia maadili ya utendaji pamoja na nidhamu serikalini, hivyo ni vizuri kutumia utaratibu huo.

“Ninyi wenyewe mmeona mfano mzuri wa Rais, tuige huu mfano, Rais hajawaji kusimama hadharani hata siku moja akamfukuza mtumishi kazi kwa kuwa anaelewa utararibu na amekuwa akizingatia utaratibu huo, tunawataka viongozi na watendaji serikalini kuzingatia utararibu hizo.

“Mfano mwingine naweza nikawapa kuna ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kuzingatia ripoti ya CAG Rais anauwezo wa kumfukuza mtu yeyote wakati wowote kwa sababu anazozijua yeye…..; “Lakini hafanyi hivyo bali husubiri utaratibu na kanuni zifuatwe kwa sababu anaweza kumfukuza au kumsema mtu hadharani lakini baadaye ikabainika hana kosa, sasa unamuombaje radhi, ” amesema

Aidha, amewataka viongozi kuurudisha utaratibu wa kuzingatia utawala bora, kuheshimu sheria, kwani hata Katiba inasema kwamba utu wa mtu ni lazima uheshimiwe na kwamba kwa kuzingatia hilo Rais Dk. Samia anaonesha mfano kwa vitendo.

Naibu Waziri wa Ardhi, GEOPHREY PINDA ametoa Mwezi Mmoja kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments