Mambo mazuri ushirikiano Tanzania, Saudi Arabia

DODOMA: MAKAMU WA Rais, DK Philip Mpango amesema uhusiano baina ya Tanzania na Saudi Arabia unaendelea kuimarika kwa mataifa hayo kushirikiana katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
DK Mpango ameyasema hayo leo Desemba 19, 2023 katika mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Yahya Ahmed Okeish, Ikulu Chamwino mjini Dodoma.
Amesema, Tanzania inatambua mchango unaotolewa na nchi ya Saudi Arabia katika ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Saudi pamoja na kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu.
Ameongeza ni muhimu mataifa hayo mawili kuongeza ushirikiano katika masuala ya biashara na uwekezaji huku akimsihi balozi huyo katika kipindi atakachohudumu nchini Tanzania kuwezesha ongezeko la makampuni mbalimbali ya Saudi Arabia kuwekeza nchini Tanzania pamoja na kuongeza idadi ya watalii kutoka taifa hilo.
DK Mpango ameipongeza nchi Saudi Arabia kupitia Balozi huyo kwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya mwaka 2030 (Expo 2030).
Amesema Tanzania imefurahishwa na uwepo wa usafiri wa ndege wa moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania ambao unaimarisha mahusiano yaliyopo baina ya mataifa hayo mawili.
Kwa upande wake Balozi wa Saudi Arabia Yahya Ahmed Okeish amesema Tanzania na Saudi Arabia zimekua na mahusiano ya kihistoria na kibinadamu ambayo yameendelea kuimarika. Ameongeza kwamba Saudi Arabia inachukulia kwa umuhimu wa kipekee mahusiano yake na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Amesema kutangazwa kwa nafasi 500 za ajira za wauguzi Watanzania nchini Saudia Arabia ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliyopo na ziara aliyoifanya Rais Dk Samia Suluhu Hassan nchini humo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments