MBUNGE wa Jimbo la Geita mjini, Costantine Kanyasu ameahidi kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita na Chama Cha Soka Wilaya ya Geita (GEDFA) kuweza kuboresha viwanja vya michezo.
Kanyasu amesema hayo wakati akihitimisha mashindano ya ligi ya wilaya ya Geita maarufu kama ligi daraja la nne yanayodhaminiwa na ofisi ya mbunge na yanafahamika kama Kanyasu Cup.
Amesema uboreshaji wa viwanja ni jambo la msingi kwa maendeleo ya soka kwani mbali na kuchagiza ukuaji wa vipaji lakini pia ni muhimu kwa ajili ya kuchangia mapato ya vyama vya soka na timu kupitia viingilio.
Kanyasu ametaja baadhi ya viwanja vya mjini Geita vinavyohitaji matengezo kwa ajili ya kuendeleza mchezo wa soka ni pamoja na uwanja wa GGML, uwanja wa Kalangalala pamoja na Uwanja wa Nyankumbu
“Lakini kama walivyosema watu wa Chama Cha Mpira wilaya ya Geita, bado hawana uwanja ambao wanaweza kuutumia kwa ajili ya mapato.”
“Sasa bila mapato hauwezi kuendesha mpira, nakubaliana na nyinyi na niwaahidi kwamba pale mtakapohitaji msaada wetu tutashirikiana tuone namna ya kufanya ili tuweze kufikia sehemu nzuri.”
Amewaomba wadau wa maendeleo mjini Geita kuunga mkono juhudi za kuendeleza mchezo wa soka kwa kudhamini mashindano mbalimbali ili kukuza vipaji na kupanua uwigo wa vijana kufikia ndoto zao.
Makamu mwenyekiti chama cha soka wilaya geita (GEDFA), Vallence Ibrahim amesema Kanyasu Cup ilijumuisha timu 12 ambapo mshindi wa kwanza alipewa Sh milioni moja na mshindi wa pili Sh laki tano.
Vallence ametaja timu zilizofanikiwa kucheza fainali ya mashindano hayo ni Shadow Fc na Geita Insititute zote za mjini Geita ambapo Geita Institute ilifanikiwa kuibuka bingwa kwa ushindi wa bao 1-0.
“Changamoto kubwa inayotukabili chama na vilabu ni kukosa wadhamini wa ligi zetu, wadhamini wakubwa wanakimbilia kudhamini ligi kuu, na kusahau maendeleo ya mpira wa miguu kwa ngazi ya chini.
“Changamoto kubwa inayotukabili ni ukosefu wa viwanja vya kuchezea na hata vya kuingiza watazamaji kwa ajili ya kupata angalau pesa kidogo ya kuendeshea pamoja na vilabu kushindwa kusajili timu zao.
0 Comments