NAONA kuna mjadala mkubwa umekuwa ukiendelea baada ya Idara ya Chipukizi ya Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya uchaguzi wa kuchagua Mwenyekiti wao Taifa sambamba na wajumbe wake.
Imekuwa gumzo sana , kumekuwa na maswali mengi, imeibua mitazamo tofauti katika jamii, wengine wanaona sawa, wengine wanasema hapana.
Basi kila mtu anasema lake, na ukweli lazima iwe hivyo , tunatofautiana katika kuwaza, kufikiria na kuamua. Pia tunatofautiana hata katika kupanga na kuamua mambo yetu, kila mtu hapa duniani ana hesabu zake.
Hata hivyo kuwa na mjadala unatokana na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Idara ya Chipukizi Taifa naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Qailah Nurdin Bilal , mtoto wa msanii maarufu nchini Sheta a.k.a Baba Qailla.
Ndio ameshinda nafasi hiyo baada ya kutoa sera ambazo zilisababisha wajumbe wa mkutano huo kumchagua kwa kishindo. Qailah ameshinda kwa kura nyingi sana.
Nilibahatika kuona video ya Qailah akiomba kura, ana uwezo mkubwa sana wa kupanga maneno, kujieleza kwa kujenga hoja. Anastahili kushinda na hakika anatafsiri maisha yake ya kesho kikubwa ni kumuombea afya na uzima ulioambatana na maisha marefu.
Hata hivyo baadhi ya wanaopingana na uchaguzi huo wanatoa sababu kadhaa na mojawapo ni kwamba watoto hao ni wadogo sana na kwa umri wao wanapaswa kuachwa wakasoma badala ya kuwaingiza katika siasa.
Sawa huenda wana hoja lakini ukweli kila mzazi ama mlezi kuna aina ya maisha au kazi anayotamani mtoto wake aje aifanye mbele ya safari. Katika kufanikisha ndoto hizo kuna njia zake, huenda za kufurahisha au kuchukiza.
Lakini katika hili la Chipukizi binafsi naungana na wazazi walioamua kuonesha njia watoto wao mapema. Wanafanya hivyo kwasababu wanajua njia hiyo inamatokeo chanya kwa watoto wao.
Sitashangaa huko mbele ya safari watoto hao mmoja wapo akawa kiongozi mkubwa wa taifa letu. Ipo mifano mingi hata sasa kuna watoto wengi wako katika uongozi aidha katika Chama au Serikali, wapo hapo kwasababu wameandaliwa mapema.
Kama Qailah ameweza kuomba kura akiwa na umri huo na akashinda , unaweza kupambana naye akiwa na umri wa miaka 25 au 30? Lazima tukubali hakuna kisichoandaliwa, huenda ishu kinaandaliwaje?
Hebu tujiulize kuna ubaya gani watoto wakionesha muelekeo wa safari yao ya maisha wakiwa wadogo? Cha kufurahisha wote wako shule na sio shule tu ni shule haswaa.Ukitaka kujua hilo angalia wazazi wao.Ni wazazi ambao wanajua nini wanakifanya kwa watoto wao.
Kuna mifano mingi ya familia ambazo zenyewe zimekuwa na utamaduni wa kuandaa watoto wao, Kabla ya kuendelea na mjadala wa Chipukizi wa CCM , naomba nitaje watu kwachache ambao waliamua kuwaandaa watoto wao mapema.
Staa wa zamani wa soka barani Afrika, Abedi Pele watoto wake wawili Andre Ayew na Jordan Ayew ni wanasoka wakubwa.
Staa wa filamu duniani, Will Smith watoto wake Jaden Smith na Willow Smith waliingia kwenye mziki na movie wakiwa na miaka chini ya 13 na mpaka leo wanafanya vema.
Pia Kheprem Thuram na Marcus Thuram. baba yao alikuwa Lilian Thuram. Kuna Daniel Maldini, yupo Empoli. Nadhani jina linajieleza na Giovanni Reyna baba yake alikipiga Sunderland pia, Claudio Reyna. Wako watoto wengi ambao wameandaliwa wakiwa wadogo na leo wametusua. Hawana presha, wanakula maisha.
Nitoe mfano mwingine wa Richard Dove Williams Jr. Baba Mzazi wa Serena na Venus William , nani ambaye hafahamu mafanikio ya Serena na Venus katika Tenisi.Wamekuwa na mafanikio makubwa na sababu ni moja tu waliandaliwa tangu wakiwa wadogo na muandaaji ni baba yao.
Vipi kuhusu Joseph Walter "Joe" Jackson, Baba wa Michael Jackson , nani hamfahamu Michael Jackson katika ulimwengu wa muziki.Jina lake katika muziki ni ngumu kufutika, dunia inamjua sababu za muziki, muziki ulitokana na uwekezaji uliofanywa na baba yake.
Hivyo wakati tunapambana kujenga hoja sio dhambi kujifunza kwa wengine na kuona watoto wao wamefikiaje mafanikio.
Najua kwa akili zetu za kubishana bishana unaweza kuniambia mbona unazungumzia watu nje ya Tanzania, basi sawa turudi nyumbani. Unamfahamu Sophia Kizigo? Unamjua?Umeshawahi kumsikia?
Sasa iko hivi Sophia Kizigo ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chipukizi pia miaka ya nyuma kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma na kabla ya hapo ameongoza wilayani zingine ikiwemo wilaya ya Mkalama mkoani Singida.
Mbunge wa zamani wa Vijana na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo aliwahi kushika nafasi kwenye Chipukizi pia. Ipo mifano mingi. Tunaweza leo tukawa tunawaona tu viongozi kama Ridhiwani Kikwete ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Jakaya Kikwete.
Niliwahi kuzungumza na Ridhiwani miaka kadhaa iliyopita, alivyoingia CCM, hakika aliingia akiwa bado mdogo sana. Sitaki kueleza sana lakini nachotoka kuelezea matokeo unayoyaona leo maandalizi yake yalianza jana.
Lakini sote tunamfahamu Joe Makini ameamua kumuandaa mtoto wake kuwa mwanasoka, amempeleka kwenye kituo vya kufundisha soka.Niwaambie tu watu wanawekeza jamani.
Mtoto wa Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba na Mtoto wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jery Silaa anayeitwa Simba Jery Silaa miongoni mwa watoto walioingia kwenye kinyang'anyiro cha kugombea uenyekiti wa Chipukizi.Una mashaka na malezi ya Dk.Mwigulu na Silaa kwa watoto wao?
Una mashaka na Msanii Sheta katika malezi ya Qailah? Ukitaka kujua mtoto ameiva sikiliza hotuba yake akiomba kwa wajumbe na akashinda kwa kishindo, ameshinda nafasi hiyo kwa kura zaidi ya 400.
Kuna wakati huwa najaribu kuangalia wanasiasa wetu nchini, nawe ukipata nafasi jaribu kufuatilia kwa makini, utabaini tunao wanasiasa ambao wameandaliwa kuwa wanasiasa na tunao wanasiasa ambao wamekuwa wanasiasa kama ajali tu, hata wanavyofanya siasa zao unajua kabisa hakuna kitu, ila ndio hivyo tena upepo umewaweka walipo.
Mwanasiasa aliyeandaliwa akiwa mwanasiasa anakaaa muda mrefu, matendo, kauli ni mienendo yake anaashiria kabisa kuna mahali ameanzia.Wapo waliompika aidha hadharani au kwa siri.
Hata hivyo nikiri kwa jinsi ambavyo CCM imeweka mifumo yake hasa ya kuandaa viongozi vyama vingine vitakuwa na kazi kubwa sana ya kupambana na CCM inapofika wakati wa chaguzi, maana wanakutana wanasiasa walioandaliwa dhidi ya wanasiasa oya oya.
Najua wako wanasiasa wa upinzani ambao wako vizuri sana lakini ukifuatilia huko nyuma utabaini waliandaliwa.Zitto Kabwe ambaye ni Kiongozi wa ACT Wazalendo akielezaa historia yake katika siasa alianza akiwa kijana mdogo sana , alianza harakati akiwa shule ya sekondari.
Leo hii Zitto anabaki kama alama ya vijana waliongia kwenye siasa na kuleta mabadiliko makubwa, siasa kupendwa na vijana.Akiwa Chadema alifanya vijana kukipenda Chama hicho na mtaji wake mkubwa ukawa ni kwa vijana.
Julius Mtatiro aliyekuwa CUF kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara na sasa ni Mkuu Wilaya Tunduru ni miongoni mwa vijana waliojiandaa wenyewe na leo yuko alikokuwa.Na hapa lazima tuelewe wapo wanaoandaliwa na wazazi kulingana na hali zao kiuchumi na wapo wanaojiandaa wenyewe.
Hata hivyo wakati naelekea mwishoni kuelezea hili narudia tena ni vema wazazi na walezi wakaendelea kuandaa watoto wao.Methali ya mkunje samaki angali mbichi ndicho tunachokiona kinafanywa na jumuiya ya Chipukizi ya CCM.
Leo hii najaribu kumuangalia mtoto wa msanii maarufu nchini Nasseb Abdull maarufu kwa jina la Diamond , Nasseb Junior anavyoandaliwa na baba yake, ameanza kumfundisha kupiga kinanda na juzi kati ameonekana akiwa naye Kigamboni tena akiwa naye jukwaani mbele ya mamia ya mashabiki wa muziki wa kizazi kipya.
Unajua nini, anachokifanya Diamond anamwambia mwanaye maisha yenye fedha yako katika muziki.Narudia tena tuandae watoto kadri tunavyoona tunaweza.Kuna wakati najiuliza kwanini familia za daktari mara nyingi watoto wao wanakuwa daktari, jibu ni moja tu wanaandaliwa aidha kwa kauli kwa vitendo.
Pia nafahamu wapo wazazi ambao wenyewe huandaa watoto wao katika kazi tofauti na wanazofanya wao.Ndio baba mwanasiasa lakini anatamani mtoto awe Rubani.Baba mkulima anataka mtoto awe daktari.Hapa ni ngumu kuona safari ya mtoto, sababu njia ziko tofauti .
Kwa mfano mtaani unakuta baba anauza bangi a.k.a ndumu na anataka biashara yake irithiwe na mtoto, atakachofanya ni kumtuma mtoto aangalie kama polisi anakuja na akiona vipi anampa akafiche chumbani kwake(chumba cha mtoto).Mtoto akikuwa unakuta anaendelea na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Ukiniuliza mimi kuhusu Chipukizi wa CCM nitakachokwambia ni muda wa kushutuka kwamba nasi tunatakiwa kuandaa watoto mapema.Tuwaandae katika elimu yao, tuwaandae kwa kile tunachotamani wawe katika maisha yao.
Tukiwa wadogo tumeimbishwa sana nyimbo za CCM tukiwa shule ya msingi, ukiuliza vipi unaambiwa tunajifunza uraia.Kupitia nyimbo zile ukijulisha na uchaguzi wa Chama kimoja , karatasi ya kura ya kumchagua Rais ina Ndio na Hapana, ukisema ndio, ndio yeye na ukisema hapana , maana yake hapana mwingine.
Unapoona leo CCM inajivunia mtaji mkubwa wa wapiga kura ni kwasababu iliwaandaa mapema wakati mwingine bila kujua tunaandaliwa kuwa wana CCM kuanzia katika mioyo yetu.
Kwa mfano tujiulize tu hivi katoto ambacho kamegombea uenyekiti wa Chipukizi unaweza kukabadilisha kirahisi kuwa CHADEMA au CUF, itabidi ufanye kazi na hapa somo kubwa kwa wapinzani ni kwamba CCM inaandaa watu wake mapema.
Hata hivyo kama hoja zangu hazijaeleweka au hujanielewa ngoja nizungumze kimtaani taani yaani, nataka kujadili kiuswahilini hivi na hapa univumilie.Iko hivi ninachokiona kelele zimekua ni nyingi kwa sababu tumeona majina ya watu maarufu katika nafasi hizo za uongozi.
Naamini watoto wa Jerry Silaaa, Mwigulu Nchemba na Balozi Mahiga wasingekuepo mjadala usingekua mkubwa.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Kashmiri na hata watangulizi wake Nimka Stanley na Gabriel Makala uchaguzi wao haukupata ukosoaji kama huu wa Qaylah na wenzake.
Wivu wa kutowaandaa watoto wetu kwa kuwasogeza karibu na ndoto kubwa kunatufanya tuchukie tunapoona watoto wa wenzetu wakishika nafasi kubwa za uongozi. Hoja ya kwamba wale watoto hawasomi ni hoja mfu kwa sababu muda wa idara ya chipukizi kufanya kazi zao ni kipindi cha likizo.
Tupunguze malalamiko. Tuandae ndoto za watoto wetu. Tuwasogeze karibu na mafanikio wakiwa angali wadogo ili wanapokuja kuwa watu wazima wawe wameshazoea uongozi ili pia wasiwe limbukeni wa nafasi watakazopata.
Ila nimewaza ujinga sana kuhusu huu mjadala wa Chipukizi wa CCM.
0 Comments