Tanzania yapepea utekelezaji Agenda ya 2063

GABORONE, Botswana: Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye utekelezaji wa  makubaliano ya Ajenda 2063, ya kuifanya Afrika kuwa mahali pa ndoto yetu kuelekea Afrika tuitakayo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko kwenye Mkutano wa kujadili utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na Wakuu wa Nchi juu ya Ajenda 2063 kwa nchi za Afrika, alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo jijini Gaborone, Botswana, ulioenda sambamba na maadhimisho ya Tamasha la KUSI.

Dk Biteko alisema kuwa,  kimsingi Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Ajenda hiyo ikiwemo  masuala ya amani, usalama na demokrasia kupewa kipaumbele kwenye  nchi, kuunganisha miradi mbalimbali ya maendeleo na nchi za Afrika ikiwemo ule wa SGR, pamoja na miradi ya umeme kupitia nchi za Kenya, Uganda, Ethiopia, na Zambia, na kufungua fursa za kiuchumi kwa nchi za Afrika.

“Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika itaendelea kutekeleza, kusimamia,na kuendeleza harakati hizi za kuifanya Ajenda hii kutimiza Dira ya Afrika tuitakayo. ” Alisisitiza  Dk. Biteko

Ajenda ya Afrika 2063 Afrika tuitakayo imebeba vipaumbele saba  ambavyo ni pamoja na kuleta Afrika pamoja kwenye masuala ya Maendeleo, kuunganisha Bara la Afrika kwenye masuala ya kisiasa kwa kutumia tunu za Afrika, Utawala  Bora na unaozingatia sheria, demokrasia, na haki, kuilinda Afrika, Afrika yenye mwelekeo wa utamaduni wake na maadili, Afrika itakayowaletea maendeleo watu wake, kwa manufaa ya wanachi wa Afrika.

Aidha Dk. Biteko alishiriki mjadala wa Marais kutoka Afrika kuhusu Ajenda ya umoja wa Afrika 2063 ijulikanayo kama Africas  Agenda 2063 inayotoa mwelekeo wa Afrika kutimiza ndoto zake na kuifanya Afrika waitakayo, mjadala uliohusisha Rais wa Jamhuri ya Watu wa Botswana, Dk. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Rwanda Dk. Edouard Ngirente akimwakilisha Rais, Paul Kagame, na Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania Dk. Doto Biteko, akimwakilisha Rais Samia suluhu Hassan.

Katika mjadala huo Dk. Biteko Alitoa tathmini ya utekelezaji wa Malengo ya Ajenda ya Afrika 2063 na tathmini ya miaka kumi ya awali kwa Tanzania, ambapo alisema kuwa Tanzania iliridhia mikataba ya utekelezaji wa Ajenda hiyo ya Afrika mwaka 2013 katika utekelezaji wa dira hiyo ya Afrika  ambapo imepiga hatua kubwa katika  uanzishwaji wa eneo huru la biashara la Afrika na kuondoa vikwazo vya kibiashara, watu na bidhaa kwa maendeleo ya Tanzania.

Ujumbe wa Tanzania ulioongozana na Dk Biteko ni pamoja na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Mudrick Soragha, Mkurugenzi wa Mipango kutoka Tume ya Mipango,  Dk. Mursali Ally Milanzi, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi Ellen Maduhu pamoja na  Balozi Edward Komba, Mkuu wa Utawala na Kaimu Balozi wa Tanzania Pretoria na anayeshughulikia Botswana.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments