WAZIRI wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, amewataka watanzania kuacha tabia ya kuhifadhi fedha majumbani badala yake watumie mabenki kuhifadhi fedha zao ili kujihakikishia usalama wa fedha zao na usalama wao
Dk Nchemba ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizundua Tawi la Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo na kushindwa kutokana na majukumu mengine ya kitaifa.
Dk Nchemba amesema ni vema wananchi wakajenga utamaduni wa kutumia benki kwa kuwa uendeshaji wa uchumi wa kisasa unategemea zaidi matuminzi ya utaratibu wa kibenki ambao kwa sasa umerahisishwa na unapatikana kwa urahisi.
“Utaratibu wa kuchimbia fedha ni utataribu wa kizamani, benki sasa zipo kiganjani kwanini uchimbie fedha? Popote ulipo unawezakupata huduma za benki,” amesisitiza waziri huyo.
Kiongozi huyo amesema Wizara ya Fedha itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na benki zote hapa nchini kama utekelezaji wa sera jumuishi za masuala ya kifedha na kiuchumi zinazolenga kuwasogezea wananchi huduma karibu hasa hizi za kifedha.
‘’Naomba kutumia fursa hii kuwaomba wafanyabiashara, watumishi wa umma na binafsi, viongozi wa Serikali wa ngazi mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuiunga mkono na kuitumia Benki ya PBZ katika shughuli zetu za kiuchumi, kwani benki hii imekuwa ikitoa huduma zake kwa uaminifu mkubwa na kwa riba nafuu.’’ Amesema Dk Nchemba.
0 Comments