Maofisa TRA wanusurika kipigo

Ni patashika, pale maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, kitengo cha ukamataji bidhaa za magendo (Fast) waliponusurika kushambuliwa na wafanyabiashara wadogo wa Holili, wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya kukamata mifuko 30 ya sukari inayodhaniwa kuwa ni ya magendo iliyokuwa imefichwa  kwenye moja ya nyumba iliyopo mjini Holili.

Inaelezwa na mashuhuda wa tukio hilo limeotokea leo Januari 12, 2024 kuwa maofisa hao waliokuwa wameambatana na askari polisi walipotaka kuchukua sukari hiyo, walizuiwa na wafanyabiashara hao ambao ni wanawake.

Kutokana na hilo, kuliibuka mvutano baina yao, huku maofisa hao wakizingirwa na wananchi walioleta vurugu wakishirikiana na wafanyabiashara.

Vurugu hizo zinaelezwa zilitishia kuwapo uvunjivu wa usalama, hivyo askari walilazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto zilizorushwa hewani ili kuwatawanya.

Imeelezwa wafanyabiashara wametumia maji kunawa nyuso zao  baada ya mabomu ya machozi kufyatuliwa.

Pia wametumia nyembe kuchana mifuko ya sukari na kuimwagia mafuta ya taa, ili kuiteketeza kwa moto.

Baada ya maofisa hao pamoja na polisi kuwadhibiti wafanyabaishara hao, imeelezwa waliondoka na mifuko minane ya sukari, huku 12 imeachwa kwa wafanyabiashara hao.

Katika eneo la tukio, gazeti hili limeshuhudia mabaki ya sukari na  makasha ya nyembe yakiwa yametapakaa kwenye eneo la nyumba ilipokutwa mifuko hiyo.

Mmoja wa wapangaji katika nyumba hiyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwenye chombo cha habari, amesema wakiwa nyumbani hapo, maofisa hao walivamia na kuingia kwenye moja ya chumba cha kuhifadhi sukari za wafanyabiashara hao na kutaka kuondoka nayo ndipo walipopiga kelele na kuzua taharuki.

"Hawa wafanyabiashara walipochukuliwa sukari yao walipiga kelele na watu walifika wa kutosha hapa, hawa wafanyabaishara hawakutaka sukari yao ichukuliwe kukaibuka vurugu,” amesema.

"Sukari mnayoina hapa imemwagika ni hawa wafanyabiashara wameichanachana ili kila mtu akose na walitaka kuimwagia mafuta ya taa," amesema.

Alipotafutwa Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, James Jilala, amesema yupo mkoani  Arusha, hivyo kumtaka mwandishi wa habari kumtafuta mkuu wa kituo cha forodha Holili, Mohammed Tukwa kwa ajili ya ufafanuzi wa jambo hilo.

"Sina taarifa ya tukio hilo, niko nje ya mkoa, naomba mtafute ‘incharge’ wa kituo cha forodha Holili kwa ufafanuzi zaidi," amesema Jilala.

Alipotafutwa Tukwa, amesema yupo nje ya kituo hicho, hivyo atafutwe mkuu wa kitengo cha ukamataji magendo mkoani, Edmund Lubinza, amekiri kuwapo tukio hilo akisema atalitolea ufafanuzi kesho, Januari 13, 2024.

"Taarifa ninayo, bado wanaendelea na kazi wakirudi ofisini nitapata ripoti.

“Huyu aliyeendesha zoezi hili ana nafasi ya kuongelea kitu kilichofanyika, siwezi kusema chochote mpaka nipate taarifa kutoka kwao, naomba nifuatili ," amesema Lubinza.

VIDEO: MVUA KUBWA YALETA MAFURIKO JIJINI MWANZA

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments