Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor H. Seff kwa pamoja na Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa wamemefanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara na mifereji iliyoharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Morogoro tarehe 27/01/2024.
Akiwa katika Kata ya Kitete, Mhandisi alitembelea barabara ya Magole Estate-Mfuru (4.5km) na katika Kata ya Mbumi Kilosa alitembelea mfereji wa maji unaosababisha mafuriko maeneo ya mjini.
“…Ndugu zetu wa Kilosa tumezunguka katika mikoa mingi ya nchi yetu tukikagua kazi zetu kuanzia mikoa ya kusini,kaskazini,kanda ya ziwa na leo tupo hapa Kilosa Morogoro ambapo Kama mnavyojua mvua zinanyesha maeneo mengi ya nchi yetu na madhara yake yapo kama yalivyo hapa lakini Nimemwelekeza meneja wa Mkoa wa Morogoro kuhakikisha Mifereji ya Maji ya Mji wa Kilosa inajengwa Mara Moja na pia niwashauri wananchi wa Mji wa Kilosa kuunda Vikundi vya Matengenezo ya Barabara (Labour Base) ili wawe sehemu ya waombaji wa kazi mbalimbali zinazotangazwa na TARURA..”Alisema Mhandisi Seff katika ukaguzi huo wa miundombinu .
Katika ziara hiyo alikuwepo pia Diwani wa Kata ya Mbumi Mhe. Shabani Amini Maringo ambaye ameishukuru TARURA chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa Mifereji ya Maji katika Mji wa Kilosa ambayo imepunguza madhara ya mafuriko kwa kiasi kikubwa katika mtaa wa Viwandani, Madaraka, Mjini, Makaburini na Shule ya Msingi Kichangani.
Mhe. Maringo alieleza athari wanazopata sasa zinatoka na maji yaliyoelekezwa kutoka kwenye matolea ya Maji ya Mradi wa SGR na kuomba TARURA kujenga Mifereji mingine ili kuyachepusha maji hayo yanayozidi kwenye mfereji wa awali pamoja na kumalizia ujenzi wa mfereji wenye urefu wa mita 750 uliochimbwa kwa nguvu za wananchi.
Mhandisi Seff amemuagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Ndyamukama kuanza mara moja usanifu wa barabara ya Magole Estate-Mfuru pamoja na ujenzi wa mifereji ya mji wa kilosa. Vilevile Mhandisi Seff aliwataka wananchi kuunda vikundi kwa ajili ya kupatiwa kazi za kusafisha barabara na mifereji ikiwa ni moja ya Sera ya Serikali ya kuwaongezea wananchi vipato na kuondokana na umasikini.
Kwa kumalizia naye Diwani wa Kata ya Kitete na Mbuni pamoja na Wananchi wameendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza Kilio chao na kumtuma Mhandisi Seff kuja kujionea mwenyewe madhara ya mvua zinazoendelea kunyesha pamoja na kutoa ahadi ya ujenzi wa barabara na mfereji.
Akiwa katika Kata ya Kitete, Mhandisi Seff alitembelea pia Shule ya Msingi ya Kitete aliyosoma Mhe. Profesa Kabudi Mwaka 1962.
0 Comments