ZANZIBAR: RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania wote kuendelea kuwashukuru, kuwapongeza na kuwaombea dua waasisi wa taifa ambao walifungua milango ya mafanikio yaliyofikiwa sasa.
Kupitia kurasa zake za mitandao Leo Januari 12, 2024 Rais Samia ametoa salamu zake za maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kuandika
“Nawatakia nyote kheri katika maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tuungane sote kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema yote aliyotujalia katika miaka hii 60. Tumshukuru kwa kutupa uhai kuishuhudia siku hii ya leo na matunda mengi mazuri ya Mapinduzi. Alhamdulillah.
Dhamira ya kujitawala wenyewe ni pamoja na kupatikana mageuzi ya kimaendeleo, Ziko shuhuda nyingi za mageuzi haya na kwa kiasi gani tumepiga hatua njema toka wakati huo mpaka sasa. Sote ni mashahidi wa hatua hizi.
Shuhuda mojawapo ni ufunguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi – Lumumba, Zanzibar. Mwaka 1976 nilikuwa mwanafunzi katika Shule ya Lumumba Zanzibar. Wakati huo, eneo ilipojengwa hospitali hii mpya ya kisasa palikuwa na zahanati ndogo kabisa iliyoitwa Miwanzini.
#ZANZIBAR: Wanajeshi walivyookoa Mateka Kwa Helkopta Uwanja wa New AMAAN pic.twitter.com/kOgiNUBGTk
— Bandola Media (@bandolamediatz) January 12, 2024
Kutoka zahanati ile ndogo hadi hapa tulipo leo ni hatua kubwa na ya kujivunia. Katika miaka hii 60 tumepiga hatua za namna hii kwa maelfu. “Ameandika Rais Samia na kuongeza
“Maendeleo ni hatua, ni jasho na damu, ni suala endelevu. Tuendelee kuwashukuru, kuwapongeza, na kuwaombea dua waasisi wetu ambao waliweka misingi ya sisi kufika hapa.
Jukumu sasa kwa kila mmoja wetu ni kutambua tulipotoka, malengo yetu kama taifa na kuendelea kufanya kazi kila mmoja kwa nafasi yake ili kupiga hatua kubwa zaidi huku tukibaki kuwa wamoja, wenye amani na utulivu. Kazi Iendelee.” Amechapisha Mkuu huyo wa nchi.
0 Comments