RAIS Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kuonesha ujasiri na utashi wa kisiasa kwa kuwa tayari kuboresha demokrasia na kutengeneza mazingira rafiki ya kufanya siasa nchini.
Wadau wa siasa na demokrasia ya vyama vingi wameyasema hayo jana katika ufunguzi wa mkutano maalumu wa siku mbili wa kutoa maoni kuhusu Miswada ya Sheria za Uchaguzi na vyama vya siasa uliofanyika Dar es Salaam.
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alisema Rais Samia kwa ujasiri mkubwa kwa lengo la kujenga na kuimarisha hali ya demokrasia, aliunda kikosikazi kilichotoa maoni mengi ya namna ya kuboresha demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.
Alisema miongoni mwa maoni yaliyotolewa ni kufanya marekebisho katika sheria za uchaguzi na zile zinazoratibu shughuli za vyama vya siasa nchini. “Kwa kuwa Rais Samia alikuwa na utashi wa kisiasa, baada ya kupokea ripoti ya kikosikazi alizielekeza taasisi mbalimbali za serikali kuanza kufanyia kazi mapendekezo hayo ikiwemo kufanya marekebisho ya sheria ambazo zinatukutanisha hapa leo (jana) hii,” alisema Jaji Mutungi.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama alisema Rais Samia anastahili pongezi kutokana na uamuzi wa kizalendo wa kujenga siasa ya nchi kwa kuzingatia mfumo wa sasa wa vyama vingi kwa njia ya maridhiano na kuvumiliana.
Jenista alivitaka vyama vya siasa nchini kwenda na Falsafa ya Rais ya R4 kwa kujenga tabia ya maridhiano na ustahimilivu katika vyama vyao ili kujenga taifa lisilo na nyufa na matabaka. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, aliwataka wadau wa mkutano huo kutekeleza falsafa ya R4 ili kuwezesha ndoto ya Rais Samia kutimia.
Aliwataka wadau hao ambao ni viongozi wa vyama vya siasa, dini, serikali, taasisi za serikali na zisizo za serikali, kujenga misingi ya uwajibikaji katika taasisi zao ili kupunguza malalamiko ya wananchi kutokana na kulegalega kwa uwajibikaji. “Ili kuanza na kumaliza tukiwa wamoja, nawasihi muwe majasiri wa kusikiliza zaidi ya kuongea na kujenga misingi ya kuaminiana ili tufanikiwe kuwa na taifa lenye umoja na mshikamano,” alisema Othman.
Aidha, aliwataka wadau hao kutoa maoni yao kwa kutanguliza uzalendo mbele kwa kutoa maoni yenye kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa na sio maoni ya kuvunja umoja wa kitaifa, ili kuwa na sheria zitakazodumu muda mrefu. Mkutano huu maalumu wa kutoa maoni kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi na za vyama vya siasa, unafanyika ikiwa ni muda mfupi tangu miswada hiyo kuwasilishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza mwaka jana.
Miswada hiyo inatokana na mapendekezo ya kikosikazi kilichoundwa na Rais Samia kukusanya maoni kuhusu namna bora ya kufanya maridhiano ya kisiasa ili kujenga taifa lenye umoja na mshikamano. Kiliwasilisha ripoti yake Oktoba 2022.
0 Comments