MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro, Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka amesema katika maisha yake ameshuhudia marais watano wakiongoza Tanzania ila hajawahi kuona Rais aliyefanikisha maendeleo kama Samia Suluhu Hassan.
Ole Sendeka amesema ameshika nyazifa mbalimbali nchini tangu enzi ya Baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere, ila hajawahi kushuhudia miradi mingi ya maendeleo kama inavyofanywa hivi sasa na Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan.
Ole Sendeka ameyasema hayo kwenye wiki ya jumuiya ya maridhiano na amani Tanzania, ambapo Benki ya CRDB imepanda miti 500 kwenye zahanati ya Nakweni Wilayani Simanjiro, kwa lengo la kutunza mazingira na kurejesha uoto wa asili.
Amesema Rais Samia amefanikisha miradi mingi ya maendeleo kwenye sekta ya elimu, afya, maji, umeme na miundombinu ya barabara, nchini kwa muda mfupi aliyoongoza nchi kuliko Rais yeyote hivyo mwaka 2025 anapaswa kuongezewa kipindi kingine cha miaka mitano.
"Nimekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kiteto kipindi cha Nyerere, nimekuwa Ofisa Tarafa kipindi cha Ally Hassan Mwinyi, nimekuwa mkuu wa utawala UVCCM Taifa kipindi cha Benjamin Mkapa, nimekuwa mbunge wakati wa Jakaya Kikwete, msemaji wa CCM na mkuu wa Mkoa wa Njombe kipindi cha John Magufuli, sijaona Rais aliyeleta maendeleo kama Samia," amesema.
Amesema wana CCM na viongozi wa vyama vya upinzani wanapaswa kujiandaa kisaikolojia wakitambua kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea kuwa Rais wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
"Nitazunguka maeneo yote ya wilaya na mikoa ya jamii ya wafugaji na kuimba mema yote na mazuri yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Ole Sendeka.
Hata hivyo, katika tukio hilo, Ole Sendeka alituzwa fedha na kalamu ya wino na maaskofu na mashekhe baada ya kughani wimbo wa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan.
0 Comments