TANESCO SINGIDA KUTATUA CHANGAMOTO YA KUKATIKA UMEME NJIA YA MANYONI.

                          
                      
Shirika la Umeme Tanzania - TANESCO Mkoa wa Singida linaendelea kufanya Ukarabati na Maboresho ya Miundombinu ya Umeme Njia ya MANYONI, inayojumuisha wilaya ya Ikungi, Itigi na Manyoni ili kuondoa changamoto ya Kukatika katika kwa Umeme wanayopata wananchi.

Meneja wa TANESCO mkoa wa Singida MWAMVITA ALLY amesema maboresho hayo ya miundombinu yatasaidia Umeme kutokukatika katika na kuwafanya wananchi waendelee na shughuli zao za kiuchumi kwenye miradi yao inayotumia Umeme.

Alisema baadhi ya miundombinu hasa nguzo za umeme zimechaka (kuoza) kutokana na kutumika kwa muda mrefu, na wakati mwingine baadhi ya wananchi wanaharibu miundombinu hiyo ya Umeme, hasa kuchoma nguzo moto wakati wakiandaa mashamba.

MWAMVITA pia ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Singida kuhakikisha wanalinda Miundombinu ya Umeme ili kuondoa changamoto ya Kukatika katika kwa Umeme  unaojitokeza mara kwa mara.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi - CCM Wilaya ya Manyoni JUMANNE ISMAIL ameishukuru serikali kupitia shirika la Umeme Tanzania TANESCO kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali za Umeme Kukatika Katika mara kwa mara.

Alisema, sio kwamba TANESCO wanapenda kukatika katika kwa Umeme kama baadhi wa wananchi wanavyodhani bali ni changamoto ambazo wakati mwingine hutokea kutokana uchakavu wa miundombinu au kuharibiwa kwa miundombinu hiyo kutokana na shughuli za kibinadamu.

 ISMAIL alisema Umeme umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa wananchi kwani, Umeme unatumika katika viwanda vidogo na vikubwa, na kwenye makazi, hayo yote yamekuwa yakiunua uchumi wa wananchi.

Kwa upande wake Mbunge wa Manyoni Mashariki Dr. PIUS CHAYA amewatoa hofu wananchi kuwa serikali imepanga kujenga Kituo cha Kupooza Umeme wilayani Manyoni, kitakachosaidia kupunguza changamoto ya Kukatika Katika kwa Umeme kutokana na kutegemea njia ya Umeme kutoka Singida mjini.

CHAYA pia amewataka wananchi kuwa wavumilivu kwa muda huu, lakini. pale Bwawa la Mwalimu Nyerere litakapokamilika changamoto hiyo ya Umeme itaisha kabisa.

Nao baadhi ya Wakazi wa Manyoni  wameishukuru serikali na TANESCO mkoa wa Singida kwa kuendelea kutatua Changamoto ya Kukatika Katika kwa Umeme kunakosababisha shughuli zao zinazotegemea Umeme kushindwa kufanyika kama inavyotakiwa.






Na Lafulu Kinala


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments