Wafanyakazi watatu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi - UNHCR nchini Tanzania wamepanda Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika, kwa lengo la kuchangisha fedha ili kusaidia uwekaji wa vifaa vya kuzuia radi katika shule zilizopo katika kambi za wakimbizi nchini Tanzania.
Safari yao ilichukua siku sita huku hatua ya mwisho ya kufikia mita 5,895 juu ya usawa wa Bahari ikianza usiku wa manane na kumalizika majira ya mapambazuko. Mvua kubwa na radi zimeleta madhara nchini Tanzania, hasa wakimbizi.
Katika mwezi mmoja pekee mwaka wa 2023, radi ilipiga shule moja katika kambi ya wakimbizi ya Nduta na kuua papo hapo watoto 5 na kuwajeruhi watoto wengine 15. Mtoto mkimbizi mwenye umri wa miezi tisa alilazimika kupatiwa matibabu ili kuokoa maisha yake baada ya kupigwa na radi katika tukio tofauti, huku mtoto mwingine mkimbizi akiachwa na majeraha ya moto mara baada ya kupigwa na radi mwezi wa Disemba.
"Wazo la kuchangisha fedha kwa ajili ya Watoto wakimbizi limetokana na sisi wapanda mlima kwa kuangazia mahitaji ya wakimbizi nchini Tanzania kwa kuzingatia umuhimu wa usalama wa wale ambao UNHCR inwahudumia hususani watoto.
Kwa kuzingatia hilo ilitubidi kuweka bidii ya kupanda mlima." alielezea Murithi M'nkubitu, mmoja wa wapandaji. Kwa Damla Balaban, ambaye ameshiriki kupanda mlima ameeleza namna ambavyo timu ya UNHCR ilikumbushwa mara kwa mara juu ya hali halisi ya maisha katika kambi nyingi za wakimbizi pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo licha ya mandhari nzuri ya mlima Kilimanjaro jambo ambalo liliwapa motisha katika safari yao yote.
“Kulikuwa na giza, baridi, na hatukuwa na usingizi wala njaa. Kulikuwa na changamoto za kimwili katika kupanda hadi kileleni lakini sikutilia shaka kama ningeweza kufanya hivyo au la, ilibidi nifanye. Hakukuwa na chaguo la kuacha, kwa sababu lengo lilikuwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya usalama wa watoto wakimbizi” alisema Damla.
“Kila nilipofikiria kuhusu watoto wakimbizi ambao wameathiriwa na radi na familia zilizopoteza Watoto wao nilipata moyo na Nguvu ya pekee ya kuendelea, kusonga mbele, na kamwe sikukata tamaa. Kupanda hadi kilele cha Mlima Kilimanjaro ilikuwa changamoto kubwa kwangu – nilipokuwa nikienda juu zaidi, oksijeni ilikuwa ikipungua, na nilipata shida katika kupumua,” aliongeza Yajun Hu.
Mabadiliko ya hali ya hewa yanaendelea kuathiri watu waliolazimika kukimbia makazi yao na jamii zinazowakaribisha na kuwahifadhi. Katika miongo ya hivi karibuni, mkoa wa Kigoma ambao uko Kaskazini - Magharibi mwa Tanzania, ambako kuna kambi za wakimbizi za Nduta na Nyarugusu - umekabiliwa na hali mbaya ya hewa kama vile joto kali, mafuriko yaliyoambatana na radi pamoja na dhoruba. Kati ya shule 56 zilizopo katika kambi za wakimbizi za Nduta na Nyarugusu nchini Tanzania, shule 46 hazina vifaa vya kuzuia radi.
Hofu ya matukio ya radi kuendelea kudhuru watoto wakimbizi ni ukweli wa kutisha kwa wakimbizi wengi na waomba hifadhi kwani Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetabiri mvua kubwa zaidi na dhoruba katika miezi ijayo. Kuweka kifaa kimoja cha kizuia radi kunagharimu takribani dola 1,700 na kinaweza kuokoa maisha ya watoto wakimbizi 1,500. "Hata hivyo, tunahitaji kuharakisha uwekaji wa vifaa vya kuzuia radi ili kulinda maisha ya Watoto wakimbizi na Jamii tunayoihudumia.
Uwepo wa vifaa vya kuzuia radi utapunguza hatari za vifo vya wakimbizi, hasa watoto. Hili ni janga linaloepukika kama kwa pamoja tutachukua hatua sasa,” amesema George Kuchio, Kaimu Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania (Uhifadhi). Kwa sasa Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi 240,000, wengi wao kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku zaidi ya nusu yao wakiwa ni watoto.
Kufikia tarehe 15 Desemba 2023, UNHCR ilikuwa imepokea asilimia 37 pekee ya rasilimali zinazohitajika ili kuweza kuwahudumia wakimbizi nchini. UNHCR inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuchangia huduma katika kambi za wakimbizi, na hasa kuchangisha fedha kwa ajili ya vifaa vya kuzuia radi katika shule za wakimbizi. Kupoteza mtoto mmoja kwa kupigwa na radi ni sawa na kupoteza Watoto wengi kwa mara moja.
0 Comments