MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amekemea wananchi kupeleka malalamiko yao ofisi ya Mkuu wa Mkoa baada ya hukumu ya mahakama kwani tabia hiyo inagombanisha mihimili ya serikali.
Shigela ametoa kalipio hilo mbele ya wadau wa mahakama mkoani Geita wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya mahakama kuu kanda ya Geita.
Amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kufuata hatua za kisheria kudai haki pale wanapokuwa hawajaridhishwa na uamuzi wa mahakama ili kuepuka kugombanisha mihimili ya serikali.
“Hukumu ikitolewa kama kuna mwananchi hajaridhika, mahala pa kwenda kuhoji ni mahakamani siyo kwa mkuu wa mkoa, siyo kwa mkuu wa wilaya na wala siyo kwa mtendaji wa kata ama wa kijiji.”
Ifahamike kuwa kwa mjibu wa Katibakama ambapo kila mhimili unafanya kazi bila kuingiliana.
Aidha Shigela amewakumbusha watendaji wa serikali kuheshimu maamuzi ya mahakama na kuzingatia misingi ya utawala bora kama ilivyoelekeza katiba ya nchi.
“Upande wa utekelezaji wa haki, wapo baadhi wanakwamisha, wapo baadhi wanataka kujadili uamuzi wa mahakama, wapo baadhi wanataka kutafsiri na wenyewe hukumu iliyotolewa.
“Nitumie nafasi hii kuwaelekeza watumishi wa serikali katika mkoa huu wa Geita, kuanzia ngazi ya kitongoji, mpaka ofisi ya mkuu wa mkoa ni marufuku kuingilia utendaji wa tuzo za mahakama.”
Amewaomba wananchi kutoa ushahidi kwa wakati ili kuisaidia mahakama itoe hukumu sahihi na kupunguza malalamiko na kuacha tabia ya kuzima ushahidi kwa makubalianoa binafsi nje ya mahakama.
“Jaji anapohukumu kwa kukosa ushahidi, lawama zinarudi kwa jaji au kwa hakimu, kwa hiyo niwasihi wananchi pale panapojitokeza makosa yametendeka, yako wazi tuzingatie haki kwa kueleza ukweli.”
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Kelvin Mhina ameliagiza jeshi la polisi kuunga mkono shughuli za mahakama kwa kuhoji watuhumiwa kwa wakati na kukamilisha upelelezi ndani ya siku 60.
Ameelekeza idara zote zinazohusika na utoaji haki kuwajibika kikamirifu ili kuisaidia mahakama kutenda haki kwa kutambua kuwa mfumo wa haki jinai ni mnyororo mrefu unaogusa idara mbalimbali.
0 Comments