DODOMA: Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesaini mkataba wa miezi sita wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 1.08 sawa na Sh bilioni 2.7 kwa ajili ya uchorongaji katika mradi wa Singida Gold Mine.
Mkataba huo umesainiwa leo Februari 16, 2024 na kushuhudiwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde.
Akizungumza mara baada ya makusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendajiw a Stamico Dk. Venance Mwasse ameiahidi Kampuni ya Shanta Mining kuwapatia huduma bora ya uchorongaji katika mradi wao wa Singida Gold Mine na kwamba uamuzi wa kuchagua Shirika hilo ni sahihi na hawatajutia.
Amesema tukio hilo ni sehemu ya mageuzi ambayo Shirika hilo linaendelea kufanya katika ushiriki wake kwenye mnyororo mzima wa shughuli za uchimbaji na utafiti wa madini.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mgodi wa Singida Gold Mine, Mhandisi Honest Mrema amesema Kampuni hiyo imeamua kuingia kandarasi hiyo na STAMICO kwa kuwa wanahitaji mashine za kisasa kwa ajili ya uchimbaji na kuendelea kufanya utafiti katika eneo lao wanalomiliki leseni na hatimaye kufikia lengo la kuwa mgodi wa kati kwa kuchoronga sana mwaka huu na ujao ili kuupanua Mgodi wa huo dhahabu wa Singida.
“Kwa historia yenu tuliyosikia hizi mita 5000 ni za kuanzia tu, tunaweza tukaongeza kiasi kutoka kwenye hizo dola bilioni 1.08 na kuwa mara tatu zaidi kutoka na matokeo ya kufanya vizuri kwasababu maeneo tunayo, pia tunaamini huu ushirikiano ni wa muda mrefu sio wa miezi sita tu,”amesema Mrema.
0 Comments