KAWAIDA AZIBANA HALMASHAURI KUHUSU FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO KWA VIJANA.

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Mohammed Ally Kawaida (MCC), amezitaka halmashauri zote nchi atakapofika huko kwenye ziara atataka kufahama jinsi ambavyo asilimia thelathini za fedha za miradi zimewasaidiaje vijana na wakurugenzi watoe takwimu za fedha hizo.

Kawaida ametoa kauli hiyo jana, katika mkutano wa hadhara wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jimbo la Same Mashariki wilayani Same mkoa Kilimanjaro.

Alisema kuwa, serikali iliamua kusimamisha mikopo ya mapato ya ndani ya asilimia kumi kwa ajili ya vijana, kinamama na Watu wenye ulemavu kutokana na sababu mbalimbali na kuyataka makundi hayo kuwa na subira kipindi hiki ambacho serikali inaangalia njia nzuri ya kukopesha fedha hizo.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya CCM alisema kuwa, Rais Samia kwa nia yake ya kuwasaidia vijana, Watu wenye ulemavu na Wanawake amekuja na jambo jingine ambapo kwa sasa miradi yote itakayokuwa ikitekelezwa katika halmashauri asimilia 70 ya fedha zake zitashushwa katika halmashauri.

Kawaida alisema kuwa, Rais amebadilisha sheria na kanuni za manunuzi zinazozitaka halmasahauri nchini kutenga asilimia 30 na kwenda kwa makundi hayo maalum ambapo watatakiwa kupewa tenda.

“Fedha hizi ni tofauti kidogo na zile za mkopo sio kwamba mnatakiwa kukopeshwa badala yake mnatakiwa kupewa tenda katika tenda za mradi husika na mkienda waambieni hao Wakurugenzi na Wenyeviti wao kwamba tenda hizi hauna masharti magumu ya kuwakandamiza kutokana na kipato chenu kuwa kidogo” alisema Kawaida.

Aidha Mwenyekiti huyo alisema kuwa, tukio lililofanywa na Mbunge wa Jimbo la Same mashariki la kuitisha mkutano mkubwa wa hadhara na kusoma taarifa ya kazi zilizofanywa na Serikali katika jimbo hilo linapaswa kuigwa na Wabunge wote nchini.

Alisema kuwa, chama cha Mapinduzi kimekuwa kikihimiza Wabunge na Madiwani kurudi kwa wananchi kuwaeleza juu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na kazi iliyofanywa na Mbunge Anna Kilango Malecel ni kazi ya kuigwa kwa Wabunge wote kutoka na kuwaeleza utekeleazaji wa Ilani.

“Ukupigao ndio ukufunzao mwaka 2015 wananchi wa Jimbo la Same mashariki mlichagua Mbunge anayetokana na upinzani hali ambayo ilipelekea Maendeleo ya jimbo kurudi nyuma na mkajifunza ambapo 2020 mkamchagua Anne Kilango na majibu ya kumchagua yeye ndio haya sasa amekuja kuwaambia kazi alizofanya kwa uaminifu mkubwa” alisema Kawaida.

Na kuongeza “Kazi hii iliyofanywa na Mbunge huyu ndio inayopaswa kufanywa na Wabunge wote kwani chama kimekuwa kikihimiza juu ya kurudi kwa wananchi na kuwaeleza juu ya utekelezaji wa Ilani wamekuwa wakieleza kwenye vikao vyetu vya Nec ngazi husika sasa tunawataka watoke na kwenda kuwaeleza Wananchi kwa kuiga mfano huu”.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecel alisema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Jimbo hilo limepokea fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo.

Alisema kuwa, kupitia wakala wa Barabara Tanroad jimbo hilo limeshapokea Bilioni 3.913 kwa ajili ya matengenezo katika barabara ya Same – Kisiwani – Mkomanzi yenye urefu wa kilomita 98 ambapo inatarajiwa kuwekwa lami yote kwa awamu ili kufungua uchumi wa jimbo hilo.

Mbunge huyo alisema kuwa, kupitia mvua za elnino zilizonyesha zimeathiri kwa kiwango kikubwa barabara na kuishukuru Serikali kwa kuanza kuleta fedhaza ukarabati wa barabara hizo ambapo jumla ya shilingi Bilioni 1.722 zimepokelewa Tanroad kuhakikisha inarejesha mawasiliano.

Aidha alisema kuwa, wakati akiingia madarakani Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jimbo hilo lilikuwa na kituo cha afya kimoja lakini kwa sasa vipo vitu vitatu ambavyo vimeshakamilika na kutoa hudumu huku pia wakitarajia kuanza ujenzi wa vituo vingine vipya viwili.TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments