Mkoa Wa Manyara Kuchunguzwa Ubadhilifu Fedha Za Miradi

BABATI: Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeielekeza Ofisi ya Rais – TAMISEMI kufanya, ufuatiliaji na  uchunguzi wa fedha walizopeleka kutekeleza miradi katika mkoa wa Manyara hasa katika miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi na kusema kuwa Kamati haijaridhishwa na ubora wa miradi na kasi ya miradi.

Kauli hiyo imetolewa na Kamati  ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kikazi katika Mkoa wa Manyara kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Babati.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ester Bulaya amesema hafurahishwi na usimamizi, ufuatiliaji, ufanisi na ubora wa miradi,  kutokukamilika kwa wakati katika mkoa huo.

“Wapo baadhi ya watumishi wanakosa uadilifu na uaminifu na kufanya fedha za serikali kama za bure ilihali zinatoka katika kodi za wananchi hii haikubaliki,”amesema.

Akitolea mfano wa  kutokukamilika kwa mradi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Babati na nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwa fedha zilishatolewa na hadi sasa miradi hiyo haijakamilika na bado Halmashauri imeomba kuongezewa fedha za kumaliza miradi hiyo.

Amesema tabia iliyozoeleka kwa baadhi ya Halmashauri zikipewa fedha  za miradi na zikimaliza fedha hizo husema zitaomba Ofisi ya Rais TAMISEMI na zitaongezewa sio sawa kwani  tabia hiyo inawalemeza na kuzitaka Halmashauri kuangalia lengo la kuanzishwa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa  na  wajue kuwa kwa vitu vidogo lazima wajitegemee.

“Haiwezekani  halmashauri inakusanya  mapato zaidi ya Sh Bilioni 3  lakini inashindwa kuchangia kuendeleza miradi ya maendeleo katika Halmashauri yake hata ya Sh milioni 30 ,  ikipungukiwa mradi hauendelei  inaomba TAMISEMI iwaletee hii haiwezekani na haikubaliki” amesisitiza Bulaya

Kwa upande  mjumbe wa kamati hiyo kwa Ally Makoa akisoma mapendekezo  kwa niaba ya Kamati imeitaka Ofisi ya Rais – TAMISEMI kufuatilia na kujiridhisha kabla haijaidhinisha fedha wanazoombwa za nyongeza kutoka Halmashauri kumalizia miradi na badala yake wafanye ufuatiliaji kwanza.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dk  Charles Msonde amesema TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Kamati kwa kuwa  wanayoyaelekeza ni kwa maslahi ya wananchi na nchi ni yao ambapo amewasisitiza Watendaji wa Halmashauri kuwa waadilifu na wafuatiliji wa miradi ya maendeleo kwa sababu wameaminiwa na Serikali.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments