GEITA; Chato. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko leo amejumuika na viongozi na wananchi mbalimbali katika misa takatifu ya kumwombea Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dk John Magufuli iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mt. Yohana Maria Muzeyi, wilayani Chato mkoani Geita.
Akitoa Salaam za Rais, Dk Samia Suluhu Hassan, Dk Biteko amesema kuwa, Dk Samia na Serikali yake inaendelea kumkumbuka hayati Magufuli si tu kama Rais katika Serikali Awamu ya Tano, bali pia kama kiongozi aliyeweka misingi mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuitekeleza.
Ametaja miradi mbalimbali ambayo ilianzishwa katika Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inaendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ni pamoja na mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP). ambao sasa umeshaanza kuzalisha megawati 235, mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam ambao tayari umeshaanza kufanyiwa majaribio na ujenzi wa Daraja kubwa la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza ambao umefikia asilimia 80.
Dk Biteko amewahakikishia Watanzania kuwa, masuala yaliyobuniwa na hayati Magufuli yanaendelea na yataendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ili kuendelea kumuenzi kwa vitendo.
“Hayati Magufuli anasifika kote duniani kwa uwezo wake wa kiongozi, karama ya kutatua matatizo ya wananchi, kuwasikiliza wananchi, kuondoa kero, uzembe, ubadhirifu, rushwa na kuhimiza uwajibikaji serikalini, nataka niwahakikishie kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayasukuma masuala yote hayo ili kutoa huduma kwa ufanisi kwa Watanzania,” amesisitiza Dk Biteko
Vilevile, amempongeza, mjane wa Hayati Magufuli, Mama Janet Magufuli kwa kuendelea kusimama kama mhimili wa familia na kuendelea kuunganisha na kuiongoza familia hiyo.
Kwa upande wake, mjane wa Hayati Magufuli, Mama Janeth Magufuli amemshukuru Rais Samia kwa kuwa pamoja na familia hiyo tangu kifo cha hayati Magufuli ambapo pia amewashukuru viongozi waliojumuika na familia katika adhimisho hilo la misa Takatifu, akieleza kuwa hiyo ni alama ya upendo kwa familia hiyo.
Naye Mbunge wa Chato, Dk Medard Kalemani amemshukuru Rais, Samia kwa kuendelea kuijali Wilaya ya Chato kwani pamoja kuitembelea Chato mara kwa mara, ameendelea kutoa fedha zinazotekeleza miradi mbalimbali kama ya maji, shule, afya ( hospitali ya kanda), barabara n.k
Amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumuenzi hayati Dk John Pombe Magufuli kwa namna mbalimbali ikiwemo kujenga makumbusho ya hayati Magufuli wilayani Chato, ambayo itafanya historia yake na kazi alizofanya kuendelea kujulikana ndani na nje ya nchi, kizazi cha sasa na cha baadaye.
Huu ni mwaka wa tatu tangu hayati, Dk Magufuli afariki dunia Machi 17, 2021. Misa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na Mbunge wa Chato, Dk Medard Kalemani.
0 Comments