TANZANIA YASHAURIWA KUENDELEA KUBORESHA MAENEO YA KIMKAKATI ILI KUKUZA UCHUMI ZAIDI

BALOZI wa Japan nchini amesema kuwa Tanzania inapiga hatua katika maendeleo ambayo nchi nyingi za bara za Asia ikiwemo Japan zimepitia hali inayopelekea kukua kwa uchumi wa Nchi na jamii kwa ujumla kutokana na uboreshaji wa miundombinu, sera za maendeleo ya viwanda, sekta ya rasilimali watu pamoja na mafunzo ya ufundi.


Akizungumza wakati wa Mkutano wa mwaka wa shirikisho la watanzania wanufaika wa program za mafunzo ya JICA ( JATA,) Balozi wai Japan nchini Yasushi Misawa amesema, Uhusiano bora baina ya Tanzania na Japan umekuwa ukichangia maendeleo ya kijamii na uchumi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya Hatua inayotekelezwa na wanachama wa JATA ambayo ina manufaa kwa watanzania kwa kuwa inalenga kutatua changamoto za kijamii ambayo ni moja ya mkakati wa JICA.

Aidha amesema kuwa katika kuyafikia maendeleo zaidi Tanzania iendelee kuboresha maeneo ya kimkakati ikiwemo viwanda, afya, mazingira, elimu na sekta muhimu kwa ujumla na kuwataka JATA kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na JICA ili kuona ni kwa namna gani wanaweza kutatua changamoto za kijamii na uchumi.

Pia ametumia wasaa huo katika kusherekea siku ya wanawake duniani kuwapongeza wanawake wa Tanzania kwa utendaji kazi uliotukuka na kueleza kuwa uhusiano wa ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Japan umelenga wanawake pia katika kuchukua nafasi sawa na wanaume.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA,) Ara Hitoshi amesema, JATA watumie fursa za jukwaa hilo kubadilishana ujuzi, uzoefu na maarifa kwa mafunzo waliyopata na hiyo ni pamoja na kujitolea ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Ameeleza kuwa uhusiano wa jukwaa hilo ni muhimu kwa JICA ambayo itaendelea kushirikiana na Tanzania kupitia Taasisi za Umma na sekta binafsi ili kuendelea kuleta matokeo chanya ya maendeleo.

" Uhusiano wa Tanzania na Japan ni imara na kupitia JICA imekuza ushirikiano huu na kupitia JATA tunaamini ujuzi mliopata kutoa mawazo, fursa na kwa jamii na kuleta matokeo yenye tija zaidi katika sekta sekta mbalimbali." Amesema.

Ameahidi kuendeleza ushirikiano zaidi kwa sasa na baadaye na kuwataka wanufaika hao kutoa fursa kwa wengine ili kutanua wigo wa fursa kwa vijana wa kitanzania.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Utumishi Leila Maviki amesema Serikali ya Tanzania inathamini jitihada za Serikali ya Japan katika kuchochea maendeleo ya Tanzania kupitia fursa za masomo na mafunzo yatolewao wa watanzania ikiwemo watumishi wa Umma ambao wamepata mafunzo kupitia JICA katika uga za afya, TEHAMA, sekta ya maji na kilimo.

Kuhusiana na utekelezaji wa miradi kupitia Hatua Project, Leila amesema miradi hiyo italeta tija kwa jamii hususani katika teknolojia ambayo watanzania wengi wakiwemo vijana watanufaika nayo.

Pia ameiomba Serikali ya Japan kuangalia vigezo vya kunufaika na program za mafunzo ya JICA ikiwemo umri kwa watumishi wa Umma pamoja na maeneo muhimu ya kimkakati yatakaoyoinufaisha Tanzania.

Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa JATA Gregory Mlay amesema kuwa shirikisho hilo limewakusanya watanzania waliopata fursa ya kusoma nchini Japan ikiwemo waliopata kupitia ufadhili wa JICA umelenga kuendeleza uhusiano wa kimaendeleo, uhusiano, ushirikiano, kubadilishana uzoefu pamoja na kudumisha uhusiano na kuendelea kufanya kazi na JICA.

Amewataka wanachama wa JATA kutumia fursa kwa kuandika miradi na kutekeleza kwa manufaa ya wananchi pamoja na kushiriki ujuzi kwa jamii.

Mradi wa Hatua ulianza mwaka 2022 kwa miradi mitano ambayo miradi miwili ilitekelezwa mwaka 2022 na mitatu ilitekelezwa mwaka 2023 kwa lengo na kupata fursa ya kutumia Teknolojia waliyoipata Japan kwa manufaa ya Tanzania.

Miradi hiyo inatekelezwa Zanzibar, Mafia na Visiga ikilenga shughuli za kilimo cha kisasa na mabadiliko ya hewa, kilimo bora cha bahari pamoja na nishati mbadala.


 

Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa akizungumza wakati wa Mkutano wa mwaka wa JATA na kueleza kuwa Serikali ya Japan kupitia JICA wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuleta maendeleo yenye manufaa kwa nchi hizo mbili. Leo jijini Dar es Salaam.
 

Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa (wa pili kulia) Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA, wa pili kushoto) wakifuatilia mada wakati wa mkutano huo. Kulia ni Mwenyekiti wa JATA Gregory Mlay na kushoto ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu Utumishi, Leila Maviki.
 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments