Miundombinu ya usafirishaji inazidi kuimarika ndani ya Mkoa wa Dodoma ambapo umeweza kupunguza wastani wa asilimia 60 za barabara zilizokuwa na hali mbaya mwaka 2020/2021 hadi kufikia asilimia 31 mwaka 2023/2024.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Edward Lemelo wakati wa mahojiano maalum na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TARURA Bi. Catherine Sungura yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dodoma.
Mhandisi Lemelo alisema kwamba TARURA Mkoa wa Dodoma imeweka lengo la kufikia asilimia 85 ya barabara zenye hali nzuri ifikapo mwaka 2025/2026.
"Tumefanikiwa kuongeza barabara zenye hali nzuri kutoka asilimia 10 mwaka 2020/2021 hadi kufikia asilimia 34.7 mwaka 2023/2024, barabara zenye hali mbaya zimepungua kutoka asilimia 60 mwaka 2020/2021 hadi kufikia asilimia 31 Mwaka 2023/2024 ”.Alisema Mhandisi Lemelo.
Alisema mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa bajeti ya kihistoria ya matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja kwa Mkoa wa Dodoma ambayo imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 12.7 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi Bilioni 34.2 mwaka 2023/2024.
“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani tangu aingie madarakani tumekuwa na ongezeko la kihistoria la bajeti kwa Mkoa wetu wa Dodoma kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja na kuendelea kufungua barabara mpya ambazo zimewezesha kufika maeneo ambayo awali hayakuweza kufikika”.
Aidha, Mhandisi Lemelo ametaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa mtandao wa barabara za lami zinazohudumiwa na TARURA kutoka Km. 171.29 mwaka 2020/2021 hadi Km. 309.71 mwaka 2023/2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 80.81.
Amesema pia kuna ongezeko la barabara za changarawe kutoka Km. 1258.65 hadi Km. 1827.5 pamoja na ufunguzi wa barabara mpya jumla ya Km. 544.60 ambazo zimefunguliwa kwa maana hazikuwepo kabisa.
“Kufunguliwa kwa barabara hizi mpya imeakisi kauli mbiu yetu ya ‘Tunakufungulia barabara kufika kusiko fikika’, miundombinu hii imewezesha wananchi kufika maeneo mbalimbali ya shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila kikwazo chochote tofauti na ilivyokuwa awali”.
Kwa upande wa ujenzi wa madaraja, makalavati, mifereji ya maji ya mvua na taa za barabarani, Mhandisi huyo alisema jumla ya madaraja 19, maboksi kalavati 45, mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa mita 73,822.24 imejengwa katika maeneo mbalimbali na jumla ya taa za barabarani 470 zimewekwa katika barabara mbalimbali za Mkoa wa Dodoma.
“TARURA Dodoma tunamshukuru Rais Samia kwa namna anavyoilea TARURA kwa kuongeza Bajeti ya matengenezo na ukarabati wa barabara inayowezesha kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya ujenzi wa madaraja, barabara za lami, kuongeza barabara za changarawe na kuendelea kufungua barabara mpya katika Mkoa wa Dodoma”.
Pamoja na hayo, Mhandisi Lemelo amewasihi wananchi kujenga utamaduni wa kutunza miundombinu ya barabara kwa hususan kusafisha mitaro na kuepuka kutupa uchafu ama kufanya mitaro kuwa jalala ili kuepuka mafuriko na magonjwa ya kuambukiza.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Dodoma unahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa Km 7,540.9.
Naye, mmoja wa dereva wa bajaji ambaye kituo chake kipo NHIF Bw. Kabila Msigara alisema sasa hivi kumekuwa na miundombinu rafiki tofauti na zamani kwani hapo awali wateja wao walikuwa wakipata shida kupanda bajaji kutokana na tatizo la kiafya pia kuna vifaa vya bajaji zilikua zinaharibika mara kwa mara kutokana na barabara mbaya ila kwa sasa mambo yamekuwa murua na wanaishukuru Serikali.
Wakati huo huo Mkazi wa Chinyoa Bi. Asnaa Marijani alisema wanamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea barabara hiyo ambapo awali bodaboda hazikuwa zinafikika katika maeneo yao kwa sababu zilikua zikikwama kutokana na ubovu wa barabara na hivyo kuwaongezea gharama za usafiri.
0 Comments