MWANZA: MADEREVA wa usafiri wa umma, maarufu ‘daladala’ wamegoma mkoani Mwanza, huku taarifa za awali zikieleza sababu ni kushinikiza kuondolewa kwa muingiliano wao (daladala) na pikipiki za miguu mitatu, maarufu ‘bajaji’, katika vituo vya kupakia abiria.
Mgomo huo umeonekana kuwaathiri zaidi wanafunzi, ambapo uchunguzi wa haraka umeonesha ni kutokana na wengi kutomudu gharama za usafiri wa bajaji,ambao umepanda kutoka Sh 700 hadi 1000.
Pikipiki za miguu miwili (bodaboda) kadhalika nazo zimepandisha nauli, hivyo kuzidisha ugumu wa usafiri.
Licha ya magari binafsi kutoa msaada wa usafiri kwa wanafunzi, bado wengi wamesalia vituoni kutokana na wingi wao.
Mwandishi wa habari hii ambaye pia ameathiriwa na hali hiyo, ameshuhudia wanafunzi hao na wakazi wengine wa Mwanza wakiamua kutembea kwa miguu kutoka eneo la Nyakato National hadi katikati ya jiji, mwendo wa takribani kilomita tano.
“Nimeamua kutembea kwa sababu licha ya kupanda kwa nauli kwa vyombo vilivyomo barabarani, bado vingi vinakuja vimejaa na ilinipasa kuwa kazini saa 1:00 asubuhi lakini sina namna.” Amesema mmoja wa wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Mgomo huo ukatoa fursa kwa bajaji na bodaboda, kutawala barabara takribani zote za Jiji la Mwanza
0 Comments