Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amesema umefika muda wa Simba kuandika historia mpya katika soka la Afrika kwa kuwaondosha Al Ahly ya Misri katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa hamasa kuelekea mchezo wa Machi 29, Ahmed amesema imezoeleka kwamba Ahly wanabadilika katika hatua za mtoano lakini safari hii Simba wanataka kuwaonesha ukubwa wao.
“Wanasema zinapofika hatua hizi Al Ahly huwa wanabadilika, sasa sisi Simba tutabadilika nao, tunataka tuone wanabadilika wapi, malengo yetu ni kumaliza kazi nyumbani katika uwanja wa Benjamini Mkapa ambapo hapa tunahitaji nguvu ya mashabiki“ Amesema Ahmed na kuongeza
Ikiwa Mashabiki watajitokeza kwa wingi uwanjani siku hiyo Ahly hana pakutokea huku akigusia simulizi nzuri ya kumbukumbu ya ushindi waliowahi kupata dhidi ya Al Ahly katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Simba watashuka dimba la Mkapa Machi 29 kuwaalika mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali kabla ya mchezo wa mkondo wa pili chini Misri.
0 Comments