KINANA APOKEA MALALAMIKO YA MAUAJI SERENGETI

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulurhaman Kinana amepokea malalamiko mbalimbali yakiwemo ya mauaji yanayotokea maeneo ya hifadhi wilayani Serengeti mkoani Mara ambapo ametumia nafasi hiyo kukemea na kusisitiza hakuna mwenye haki ya kukatisha uhai wa mwingine.

Akizungumza leo Aprili 14,2024 katika kikao cha ndani kilichowakutanisha wanachama wa Chama hicho Wilaya ya Serengeti mkoani Mara Kinana ametumia nafasi hiyo kueleza kuna kila sababu ya viongozi kuwaelimisha wananchi kuheshimu mipaka iliyopo sambamba na kukemea mauaji.

“Mkuu wa wilaya ya Serengeti amelifafanua vizuri sana na huwezi kuulaumu upande mmoja peke yake, lakini tunawajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu kuheshimu mipaka lakini jambo moja la msingi hakuna mwenye haki ya kuondoa uhai wa mtu. Hata katika Katiba haki ya kwanza ni kuishi,” alisema.

Amefafanua serikali hairuhusu kukatishwa kwa maisha ya mwananchi yeyote na vyombo vya ulinzi na usalama wajibu wake ni kufuata sheria.

Aidha amesema katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo tayari Serikali imeunda kamati ndogo ambayo itafika mkoani Mara kufanya tathimini na hatimaye kutatua changamoto hiyo.

Kabla ya kuelezea hayo baadhi ya wana CCM akiwemo Diwani wa Kata ya Machochwe Joseph Magete walimwambia Kinana kumekuwepo na matukio ya kutatanisha pembezoni mwa hifadhi hiyo kwa watu kupotea, hivyo wamemuomba kuangalia suala hilo kwa nini linatokea katika hifadhi.

Kuhusu kero ya mpaka kati ya wilaya ya Serengeti na Bunda Kinana amesema kabla ya kufika katika kikao hicho amezungumza na Kamati ya Siasa ya Wilaya na ameelezwa changamoto hiyo imekuwepo kwa zaidi ya miaka 50.

“Nikajiuliza kwa nini liwepo wakati watu wa Bunda na Serengeti ni ndugu na kwa kuwa wazee wapo watatuongoza katika hili.

"Nitashauriana na viongozi wa Mkoa wa Mara pamoja na viongozi wa kitaifa. Kwa mtazamo wangu hili jambo ni la kijamii si la kiserikali,” alisema.

Amefaafanua kabla ya kutenganishwa Wilaya ya Bunda na Serengeti ilikuwa moja na inawezekana kugawa watu, lakini huwezi kugawa undugu.

Hata hivyo amesema ni vema wazee wakae washauri lakini umefika wakati wa kutafuta namna nzuri ya kutatua kwani njia inayotumika sasa sio nzuri maana haiwezekani kwa muda wote huo ishikandikane.

Kuhusu barabara inayounganisha Sanzati, Nata hadi Arusha yenye urefu wa kilometa 40, Kinana amesema mepokea kero hiyo na tayari amezungumza na Waziri wa Ujenzi Inocent Bashungwa kuhusu ujenzi wa barabara hiyo.

“Waziri wa Ujenzi atakuja kwa ajili ya kusimamia barabara hii.Haiwezekani jambo hili tuwe tunajadili kila mwaka na kuahidi halafu isitekelezwe, hivyo nitasimamia kuhakikisha barabara inakamilika.”


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments