UHAI na uimara wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika tafiti, utoaji wa huduma za ushauri wa kitaalamu pamoja na huduma za ugani umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji na tija katika Sekta ya Kilimo nchini.
Kauli hiyo imetolewa Aprili 8, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Doto Biteko wakati akimwakilisha Rais wa Zanzibar Mh. Hussein Mwinyi kwenye ufunguzi wa Mdahalo wa kitaifa wa Kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika mjini Morogoro.
Dkt. Biteko amewaasa Viongozi wa kuendelea kutoa mafunzo ya kuzalisha wataalam wenye ujuzi katika sekta ya kilimo na mifugo na kuifanya sekta hiyo iwe kimbilio la watu wengi hasa vijana ambao ndio nguvukazi ya taifa.
Amesema iwapo SUA wataendelea hivyo watakuwa wanaendelea kumuenzi kwa vitendo Hayati Sokoine ambaye amebeba jina la Chuo hicho kwa kuwafanya vijana wakaigeukia sekta ya kilimo kama chanzo cha ajira na chanzo cha kukuza Uchumi wao.
Akizungumzia maisha ya Hayati Sokoine, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema Kiongozi huyo alikuwa ni mzalendo mwenye uadilifu, shujaa na asiyekuwa na mzaha katika utendaji kazi ambapo matokeo ya kazi zake yalionekana kwa vitendo sio maneno.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda amesema Kauli Mbiu ya Kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Sokoine ni Urithi wa Taifa katika Uongozi wake, bidii, uadilifu na uamifu ambayo inaakisi hali halisi ya maisha ya Hayati Sokoine.
Prof. Chibunda amesema Kauli mbiu hiyo inalenga kuwezesha vijana kuenzi historia, urithi usiofutika na misingi imara ya uongozi iliyoachwa na Hayati Sokoine ambayo itatumika kama rejea ya kuongoza vijana na vizazi vya sasa na vijavyo.
Wachokozaa mada katika mdahalo huo walikuwa ni Spika wa Bunge Mstaafu Mhe. Anna Makinda, Profesa Mstaafu wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Prof. Issa Shivji, Jaji Mstaafu Mh. Joseph Sinde Warioba na Prof. Kalunde Sibuga kutoka SUA ambao wote katika maelezo yao wamemuelezea Hayati Sokoine kama Kiongozi wa mfano wa kuigwa ambaye alikemea rushwa na vitendo vya uhujumu uchumi.
0 Comments