RC SENYAMULE AZINDUA BONANZA LA MICHEZO DUWASA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo Mei 04,2024 amezindua Bonanza la Siku ya Michezo ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) lenye lengo la kuhamasisha wafanyakazi kushiriki michezo na kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.


Mhe. Mkuu wa Mkoa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Bonanza hilo ameshiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa Pete (Netball) na ameipongeza DUWASA kwa kutekeleza Agizo la Serikali la kuhakikisha Taasisi zinaanzisha, kusimamia na kutekeleza dhana ya michezo kwa Viongozi na watumishi.

Aidha, Mhe. Senyamule kupitia Bonanza hilo la DUWASA ametoa maagizo kwa Taasisi zote za umma mkoa wa Dodoma kutekeleza maagizo ya serikali ya watumishi kushiriki mazoezi na michezo kwa ajili ya kulinda afya na kujiandaa kushiriki Mashindano ya SHIMUTA ya mwaka huu.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya DUWASA amewaasa watumishi kubadili mienendo ya maisha inayohatarisha afya zao hali inayoweza kudhoofisha ufanisi wa kazi.

Akizungumzia malengo ya kufanyika kwa Bonanza la Siku ya Michezo, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema ni utekelezaji wa maagizo ya serikali pamoja na DUWASA kuhakikisha watumishi wanakuwa na afya njema wakati wa kutekeleza majukumu yao na itawasaidia kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari na shinikizo la damu.

Katika Bonanza hilo watumishi wa DUWASA wameshiriki michezo mbalimbali, ikiwemo mbio fupi, mpira wa Pete na miguu, kufukuza kuku, riadha na mbio za magunia ambapo washindi wamezawadiwa vikombe vya ushindi na fedha taslimu.

Uzinduzi wa Bonanza la Siku ya Michezo DUWASA limefungua mwendelezo kwa watumishi wote kushiriki mazoezi kila Ijumaa ya kila wiki baada ya muda wa kazi.













TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments