Samia awashika mkono waathirika mafuriko Mkuranga

PWANI; RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa msaada wa jumla ya tani 19 za chakula na mahitaji muhimu kwa waathirika wa mafuriko katika kaya 72 zenye watu zaidi ya 300, wilayani Mkuranga,mkoani Pwani.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Rais Samia, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega, alipowatembela waathirika hao jana katika kata za Kisiju, Dondo na Magawa, amesema, msaada uliotolewa na serikali ni pamoja na mchele, unga, sukari, mafuta maharage na magodoro.

Amesema Rais Samia, ameguswa na changamoto ya mafuriko iliyowakuta wananchi wa wilaya hiyo ambapo ametoa msaada wa  mchele tani 4, unga tani 5 na maharagwe tani 10 katika kata hizo katika vijiji vya Kerekese,Kalole,Mavunja na Kisiju Pwani.

“Rais Samia anawapa pole sana kwa changamoto hii iliyowapata na ametoa chakula ambapo kila kaya itapata kilo 10 za mchele, kilo 5 za unga na kilo 5 za maharage pia kuna magodoro ambayo kila kaya itapata moja pia Sukari, mafuta, ndoo za maji,  na sabuni”amesema Ulega

Ulega amesema mbali na serikali kutoa msaada huo pia imetoa fedha kiasi cha Sh milion 720 kwa ajili ya kutengeneza barabara zilizokatika na kuathiriwa na mafuriko jambo ambalo litasaidia kuondokana na adha iliyopo kwa sasa.

“Msaada huu ni wa serikali na ni matumaini yangu viongozi mtasimia shughuli ya ugawaji vizuri  na mhakikishe vinaenda kwa walengwa, maafa ya mafuriko yametokea nchi nzima na yameleta maafa makubwa na kuharibu miundombinu yetu ya barabara lakini mbali na kutoa chakula pia serikali imetuletea zaidi ya Sh milioni 700 kwa ajili ya ukarabati wa barabara zetu”amesema

Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Ally Nasri, amesema  mafuriko hayo yameta athari kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo ambapo baadhi wamepoteza makazi  yao.

Halima Lmao ambaye ni muathirika wa mafuriko hayo, aliishukuru serikali kwa msaada huo na kwamba changamoto iliyopo kwa Sasa ni ukosefu wa huduma za afya karibu ambapo aliiomba serikali kutatua changamoto hiyo.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments