SERIKALI KUJENGA KITUO CHA KUPOZEA UMEME WILAYANI MANYONI : DKT.NCHIMBI

                           

Katibu Mkuu wa CCM Dkt. EMMANUEL NCHIMBI amesema Serikali itajenga Kituo Kidogo cha Kupooza Umeme wilayani Manyoni ili kupunguza kero ya kukatika katika kwa Umeme wilayani humo, ili wananchi waweze kupata huduma mbalimbali za Kijamii ambazo hutegemea Umeme.


Dkt NCHIMBI alisema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida akiwa katika Ziara yake ya kuimarisha Chama,  kupokea Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM Singida na Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Alisema ili kutatua changamoto hiyo serikali itajenga kituo hicho kidogo cha Kupooza Umeme na wananchi wapate huduma zote zinazotokana na upatikanaji wa Umeme.
                        

Hata hivyo aliwataka wananchi kuacha kufuata maneno ya wanasiasa wanaochochea masuala ya kutaka kuligawa taifa kwa visingizio vya kuwa Muungano wa Tanzania Bara na Visiwani hauna faida, Muungano ambao umedumu kwa muda mrefu na umekuwa wa kuigwa barani Afrika na Duniani kote.

Dkt. NCHIMBI alisema watu hao wapuuzwe kwani wanachochea uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini.
                              

Alisema watu hao wakitoka kwenye suala la Utanganyika na Uzanzibari, watahamia kwenye kufarakisha kwa kuwagawa wananchi kupitia makabila yao, jambo ambalo hakikubaliki litokee hapa nchini.

Dkt. NCHIMBI pia aliwataka wananchi kuwaonesha wazi wazi wanasiasa hao kuwa hawapendezwi  wala hawafurahishwi na maneno yao hayo ya uchechezi yanayoweza kuleta uvunjivu wa Amani na Utulivu nchini.

                            
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida MARTHA MLATA aliiomba Serikali kujenga Kituo Kidogo cha Kupooza Umeme katika Wilaya ya Manyoni ili kuondoa au kupunguza changamoto ya kukatika katika kwa Umeme.

MLATA alisema changamoto hiyo kukatika katika Umeme kunasababisha kukosekana kwa huduma ya upatikanaji wa Maji Safi na Salama kutokana na kukosekana kwa Umeme wa uhakika ambao unasababisha visima vya maji kushindwa kutoa maji pale Umeme unapokatika.

Alisema kuwa hata huduma zingine za kijamii wananchi wamekuwa wakishindwa kuzipata kwa wakati kutokana na changamoto hiyo ya kukatika katika kwa Umeme wilayani humo.

                              

Pamoja na changamoto hizo MLATA aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Singida.

MLATA alisema ili kumlipa fadhila Rais Dkt SAMIA kwa maendeleo aliyoyaleta Singida ni kuwa watamlipa katika sanduku la kura katika chaguzi zijazo za serikali za Mitaa utakaofanyika Mwaka huu na uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa kukipigia kura nyingi Chama cha Mapinduzi -CCM. 

                                    
Mkuu wa Mkoa wa Singida HALIMA DENDEGO alisema Viongozi wa Chama na Serikali wanashirikiana vizuri ili kutimiza malengo ya kuwafikishia wananchi huduma.

Katika suala la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu DENDEGO alisema Mkoa wa Singida umejipanga Kuhamasisha wananchi wanajitokeza kwa wingi kuchukua Fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Alisema kila mwananchi ana Haki ya kuchagua na kuchaguliwa, hivyo aliwataka wananchi wahakikishe wanashiri kwa ukamilifu katika Uchaguzi huo.

                                      
Kwa upande wake MNNEC wa Mkoa wa Singida YOHANA MSITA alimshukuru Rais Dkt SAMIA SULUHU HASSAN kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wa mkoa wa Singida kwa kutekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo hasa Wilaya ya Manyoni.

Pamoja na shukrani hizi MSITA alisema wilaya ya Manyoni bado inakabiliwa na changamoto ya kukatika katika kwa Umeme hali inayosababisha wananchi kushindwa kufanya shughuli za maendeleo kwa wale wenye viwanda vidogo.

Hivyo aliiomba serikali kujenga kituo kidogo cha kupoza Umeme wilayani Manyoni ili kuondoa au kupunguza changamoto ya kukatika katika kwa Umeme.

Hata hivyo MSITA aliiomba serikali pia kutoa ruksa ya wananchi kufanya shuguli za uchimbaji wa madini ya dhahabu yaliyopo katika hifadhi ya mapori ya akiba ya Magesi na Rungwa ili wananchi wa Manyoni wainue vipato vyao na taifa kwa ujumla.
                           
Kwa upande wao Wananchi wa wilaya ya Manyoni walikiri kuwa kuna changamoto kubwa ya upatika
naji wa huduma za Maji safi na Salama kwa kipindi cha Muda mrefu, hivyo waliiomba serikali kutatua changamoto hiyo ya Maji.

Walisema changamoto hiyo ya ukosefu wa Maji katika wilaya ya Manyoni inasababisha wananchi kutumia muda mrefu kufuata Maji na kushindwa kufanya shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments