Shigella: Wanawake muungeni mkono Samia

GEITA: RAIS Samia Suluhu Hassan ametajwa kuvunja minyororo ya mifumo dume na ameonesha uwezo mkubwa, hivyo wanawake wanapaswa kumuunga mkono.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella usiku wa kuamkia leo Mei 27, 2024 katika hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa na Jukwaa la Wanawake wilayani Mbogwe likiwa na lengo la kuunga mkono juhudi na kazi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mrtine Shigella katika hafla maalumu mkoani humo.

Shigella amesema wanawake wanapaswa kujiamini na kutumia fursa mbalimbali zinazowazunguka ili kujiimarisha kiuchumi badala ya kuendelea kulalamika kukwamishwa na mfumo dume.

“Hamtakiwi kuwa wanyonge tena, mjiamini kwani hakuna mfumo dume kwa sasa, wanawake mnaweza  na hilo limedhihirishwa na Rais wetu Mhe. Rais Samia, ndiyo maana baada ya kuingia madarakani amepata tuzo mbalimbali kutokana na uchapaji kazi wake,”amesemaShigela.

Aidha, amewataka viongozi wa Mbogwe wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Sakina Mohamed, Katibu Tawala wa Wilaya, Dk Jacob Julius (JaJu) na Mkurugenzi Mtendaji, Saada Mwaruka kuaminiana na  kuheshimiana ni msingi wa uongozi madhubuti na unafanya hata  Rais aliyeteua aone kuwa hakika hakukosea uteuzi.

Amesema, Rais Samia Suluhu Hassan hakukosea katika uteuzi wa viongozi aliowapeleka Mbogwe kwani katika Wilaya ambazo hazimnyimi usingizi ni Mbogwe kutokana na ushirikiano, kuheshimiana, uimara, ubunifu na uthubutu wa viongozi wake.

Amesema viongozi wa Wilaya ya Mbogwe wanaonesha mfano halisi wa namna ushirikiano na kuaminiana kunavyopaswa kuwa baina ya viongozi walioaminiwa.

Shigella amekuwa RC wa mkoa huo tangu Agosti 2022 akiteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, huku mtanglizi wake akiwa Rosemary Senyamule aliyehamishiwa Mkoa wa Dodoma.

Wakati wa mapokezi yake mkoani Geita, Shigella alisema vipaumbele vyake kama alivyotakiwa na mteuzi wake, Rais Samia ni kutatua chagamoto za wana Geita, sanjari na kukusanya mapato ya kutosha.

Mnamo Agosti 25, 2022 katika mkutano wake na viongozi wa dini, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na baraza la wazee, Shigella alizungumza na makampuni makubwa mkoani humo na kuwakumbusha kuwa serikali ilianzisha utaratibu wa kampuni kubwa zinazojihusisha na uchimbaji wa madini kutoa CSR ili kusaidia wananchi kwenye maeneo ya uchimbaji waweze kunufaika hivyo ni lazima matunda yaonekane.

“Mkoa wetu na hasa kwenye halmashauri hizi mbili (halmashauri ya mji na halmashauri ya wilaya ya Geita) wanapata Sh bilioni 9.2 kila mwaka. Ni fedha nyingi sana.

“Tutaweka msukumo kwenye hizi fedha, zilete athari zinazoonekana. Hatuwezi kuwa na shilingi bilioni tisa stendi yetu ikaendelea kuwa ya vumbi.

“Hata kama tunajenga stendi kubwa basi tujenge ile stendi ya sasa iwe ya daladala, iwe ya kisasa zaidi, hatuwezi kuwa na shilingi bilioni tisa tukawa hatuna mitaro ambayo inapitisha maji.

“Wakati mwingine hizi fedha zinaonekana kama siyo fedha za umma, lakini hizi ni fedha za umma. Serikali imetunga sheria, ndio maana tunataka zilete maendeleo kwenye maeneo yetu, kwa hiyo nataka niwahakikishie jambo hili tumelibeba kwa uzito unaostahili,” alisisitiza.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments