Sasa aliyekuwa Kiungo wa Wanamsimbazi na Young Africans Haruna Moshi ‘Boban’ amewataka matajiri wa klabu hiyo, wafanye kitu kwa staa huyo,
Boban ambaye aliitumikia Simba kwa takribani miaka nane huku pia akifanikiwa kuichezea Yanga, amesema kuna umuhimu wa Kibu kuendelea kusalia Simba.
“Kuna umuhimu Kibu kuendelea kusalia Simba, licha ya timu hiyo kupita kwenye upepo mbaya lakini ni mchezaji anayejitolea muda wote kuhakikisha wanapata matokeo mazuri, anakaba na kushambulia, ana kasi na nguvu, kifupi anacheza soka la kisasa,” amesema na kuongeza;
“Ni adimu kumkuta mchezaji wa aina yake akawa na vitu vyote hivyo, Kibu asiangaliwe kwenye kufunga tu, ana vitu vingi vyenye faida kwenye timu, mshambuliaji ni ngumu kumkuta anakaba ila Kibu anafanya hivyo.
“Cha kufanya viongozi wa Simba wamsajilie mafundi zaidi ambao watampunguzia baadhi ya majukumu ya namna anavyonyambulika uwanjani, naamini kumbakiza Kibu lipo ndani ya uwezo wao, Simba ni kubwa.”
Amesema inachopitia Simba kwa sasa kiwafanye wajue wapi walikosea kisha wajipange upya kwani anaamini misimu inayokuja itatikisa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Simba ni kubwa na kinachoendelea ni kipindi cha mpito, kikubwa viongozi wajue ni wapi pamewakwamisha kisha warekebisha, watafanya makubwa zaidi,” amesema.
Kwa mtazamo wake binafsi, nje na kuingilia majukumu ya kocha anaona Simba inatakiwa kusajili beki mmoja wa kati, kiungo na washambuliaji.
“Najua hiyo ni kazi ya kocha ila kama binadamu yoyote anayetazama mpira na nimecheza naona maeneo hayo ni muhimu wayaongezee nguvu.”
DATA ZA KIBU DENIS MSIMU HUU
Msimu huu kafunga bao moja dhidi ya Yanga katika Ligi Kuu Bara Simba ilipofungwa mabao 5-1 wakati msimu uliopita alimaliza na mabao matatu na 2021/22 alimaliza na mabao manane na ndio ulikuwa kwa kwanza kuitumikia timu hiyo akitokea Mbeya City.
0 Comments