Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ALLY HAPI amewataka wananchi kuacha kuwafuata wanasiasa wanaofanya Siasa Chafu ambazo zinaleta chuki ikiwa ni pamoja na Udini na Ukabila ili kuvuruga amani iliyopo nchini.
HAPI alisema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Manispaa ya Singida akiwa katika ziara yake ya kuimarisha Jumuiya hiyo na Chama cha Mapinduzi CCM mkoani Singida.
Alisema kuna baadhi ya wanasiasa wanafanya Siasa za kutaka kuvuruga amani iliyopo kwa kueneza siasa chafu ambazo hazina faida kwa Taifa.
HAPI aliongeza kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wanasema kwanini Rais Dkt SAMIA SULUHU HASSAN anafanya maamuzi na wakati yeye ni Mzanzibari na sio mtu kutoka Tanzania bara.
Alisema watu hao wapuuze kwani Tanzania imetokana na muungano wa nchi mbili Tanganyika na Zanzibar na hivyo Rais SAMIA ameshika madaraka kutokana na Katiba ya nchi inavyoelekeza.
Aidha alisema hata hivyo Vyama vingi vilianzishwa na Rais ALLY HASSAN MWINYI mwaka 1992, hivyo basi kama wanaona Rais Dkt. SAMIA hatakiwi kufanya maamuzi na wakati ni Rais wa nchi hii, basi na Vyama vyao vifutwe kwani uamuzi wa kuanzishwa Vyama vingi ulitolewa na Rais MWINYI kutoka Zanzibar.
Hivyo HAPI aliwataka wananchi waendelee kumuunga mkono Rais Dkt SAMIA SULUHU HASSAN kwa maendeleo anayoyafanya nchini kupitia Miradi mbalimbali inayotekelezwa.
Alisema Rais Dkt SAMIA ametatua changamoto nyingi kwa wananchi kwa kusogeza huduma za kijamii katika maeneo yao, hata hao wanaohubiri siasa chafu pia wanapata huduma hizo.
0 Comments