Mkuu wa Mkoa wa Singida HALIMA DENDEGU amepiga Marufuku wanafunzi kukuaa chini baada ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Bomani Manispaa ya Singida kuonekana wakifanya mitihani wakiwa wamekaa chini kutokana Shule hiyo kukabiliwa upungufu wa Madawati.
DENDEGO alitoa agizo hilo wakati akizungumza na Walimu na Watendaji wa Manispaa ya Singida katika Shule hiyo ya Msingi Bomani, alipoitembelea shule hiyo kufuatia taarifa zilizosambaa mitandaoni zikionesha wanafunzi wakifanya Mitihani wakiwa wamekaa chini.
Alisema suala hilo halikubaliki kwani serikali imefanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya shule ili wanafunzi wapate Elimu wakiwa katika mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia.
Kutokana na changamoto hiyo DENDEGO aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Singida kuhakikisha wanaondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini katika shule zote za Msingi mkoani humo, ili kuwasaidia wanafunzi kusoma wakiwa katika mazingira rafiki.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa DENDEGO alitoa siku Saba (7) kwa uongozi wa Manispaa ya Singida kuhakikisha Madawati Nane (8) ambayo ndio upungufu uliopo shule hapo, yanapatikana kwa kipindi cha siku hizo Saba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida GODWIN GONDWE alisema watahakikisha wanaondoa changamoto hiyo ya wanafunzi Kukaa chini kwa kufanya ufuatiliaji wa shule zote za Wilaya hiyo.
GONDWE pia akaahidi kuwa uhaba wa Madawati hayo Nane (8) katika Shule hiyo ya Bomani utatatuliwa haraka iwezekanavyo kwa kufuta maelekezo ya Mkuu wa Mkoa.
Naye Mwl. Mkuu Shule ya Msingi Bomani, JOACHIM MSECHU alikiri tukio hilo kutokea la wanafunzi kukaa chini wakiwa wanafanya mitihani, na kusema kuwa haikuwa kwa nia mbaya.
Alisema wamekuwa wakifanya utaratibu wa kuwaweka wanafunzi mmoja mmoja kila Dawati na wanaobaki hukaa chini kwa utaratibu huo huo wa kukaa mmoja mmoja wakati wa kufanya Mitihani ili kuondoa changamoto ya kuigiliziana majibu.
MSECHU alisema shule hiyo ina Madawati ya kutosha na inakabiliwa na upungufu wa Madawati Nane (8) tu, ambapo alisema watahakikisha Madawati hayo yanapatikana ili kuondoa changamoto hiyo ya wanafunzi Kukaa chini.
0 Comments