MTANDAO wa Kupinga Utumikishaji Watoto Tanzania, umesema watoto wa kiume ndio waathirika wakubwa wa kutumikishwa kazi katika jamii.
Pia umesema watoto hao wamekuwa wakitumikishwa zaidi katika Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mwanza kutokana na kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi.
Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam Mei 30,2024 na Mwenyekiti wa bodi ya Wakurungezi wa Mtandao huo, Dkt. Katanta Siruwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Utumikishaji Watoto Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 12.
Amesema utumikishaji wa watoto hapa nchini Tanzania bado ni chagamoto kubwa ndio maana Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau kuchukua hatua stahiki zaidi.
"Pamoja na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa bado zipo chagamoto kadhaa ikiwemo watoto kuendelea kufanyishwa kazi ngumu katika maeneo ya kazi ya ndani,mashambani, mitaani na migodini huku takribani watoto millioni tano nchini Tanzania yaani mtoto mmoja kati ya watoto wanne wapo katika ajira,"amesema Dkt Siruwa.
Amesema ajira hizo zimekuwa kichocheo cha utumikishaji na ukatili dhidi ya watoto ambapo baadhi yao kukosa masomo na kunyanyaswa kiuchumi kwa kuwa hulipwa ujira mdogo na kusababisha kupata matatizo ya kifya na kuathiri ukuaji wao.
Akitaja sababu ambazo zimekuwa zikichagia utumikishaji watoto ni umasikini pamoja na jamii kukosa uelewa juu ya madhara ya utumikishaji.
Dkt. Siruwa amesema kupitia mtandao huo wataendelea kuhamasisha jamii kuheshimu haki za binadamu katika masuala ya kazi na ajira.
Aidha alitoa wito kwa Serikali na wadau kuunganisha nguvu ya pamoja kupinga utumikishaji watoto mahali popote.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Ibrahim Samata amesema utumikishaji wa mtoto katika kazi hatarishi unaathiri afya na maendeleo ya watoto na kuwakosesha fursa ya kupata elimu na maendeleo yao kimwili, kiakili na kiustawi.
Amesema zipo sekta zimekuwa zikiongoza katika Utumikishaji wa watoto ambazo ni pamoja na kilimo asilimia 8.7, uchimbaji madini asilimia 0.4, maji asilimia 0.6, ujenzi asilimia 0.3 na biashara asilimia 6.5.
Aidha Mratibu wa kitaifa wa Mtandao huo,Bi Scholastica Pembe amesema kwa mwaka huu maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika mkoani Simiyu .
Amesema katika kuelekea Maadhimisho hayo mtandao huo kwa kushirikiana na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu wamepanga kutekeleza shughuli mbalimbali.
0 Comments