KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU MWAKA 2024 AFURAHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI CHITOHOLI

Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 225,000 juu ya ardhi ambalo litahudumia wakazi wa vijiji mbalimbali katika kata ya Chikongola na Mkundi wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.
Ofisi ya Jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO)iliyojengwa kupitia mradi wa maji safi na salama wa Chitoholi wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Chitoholi kata ya Chitoholi wilayani Tandahimba wakisubiri Mwenge wa Uhuru kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji safi na salama unaotekelezwa na Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 1.484.


Na Mwandishi Maalum, Tandahimba
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mnzava,ametoa pongezi hizo jana baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Chitoholi kata ya Chitoholi wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara unaotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilayani Tandahimba.

“Naipongeza sana Serikali ya awamu ya sita chini ya Mama yetu Rais Dkt Samia kwa kazi kubwa inayofanya ikiwa ni pamoja na kutoa fedha nyingi za ujenzi wa miradi ya maendeleo,tumejiridhisha na nyaraka za mradi huu baada ya kuzikagua,hivyo Mwenge wa Uhuru umekubali kuweka jiwe la msingi”alisema Mnzava.

Katika hatua nyingine Mnzava amewataka wananchi wa kijiji cha Chitoholi na vijiji vyote vinavyotarajia kunufaika na mradi huo,kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji vilivyopo ili viweze kuzalisha maji kwa wingi ajili ya kuendesha mradi mradi huo uliojengwa mahususi kwa lengo la kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwao.

Amewakumbusha juu ya umuhimu wa kulinda miradi na miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa ya fedha za serikali ili miradi hiyo iwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Alisema,Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anataka kuona kila mwananchi anapata huduma ya maji umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yake ili kuwapa nafasi ya kujikita zaidi kwenye shughuli zao za mendeleo badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Mnzava,amewapongeza wataalam wa Ruwasa kwa kutumia mfumo sahihi wa manunuzi katika utekelezaji wa mradi huo na kwa kujenga kwa viwango vinavyoendana na fedha zinazotolewa na Serikali.

Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tandahimba mkoani humo Mhandisi Antidius Muchunguzi alisema,mradi huo unatekelezwa ili kuondoa adha ya upatikanaji wa maji safi na salama katika vijiji sita.

Amevitaja vijiji hivyo ni Chitoholi A na B,Mikunda shuleni,Mikunda sokoni,Dinembo na Lubangala vyenye wakazi wapatao 10,947 ambao ni sawa na asilimia 4 ya wananchi wote wa wilaya ya Tandahimba ambao awali walikuwa wanapata maji umbali kati ya kilometa 8 hadi 10 kwenda na kurudi.

Muchunguzi alisema,mradi wa maji Chotoholi umetengewa jumla ya Sh 1,484,878,497.19 na unahusisha ujenzi wa nyumba ya mashine,nyumba ya mlinzi na ujenzi wa ofisi ya Jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO).

Alitaja kazi nyingine zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita 225,000,ununuzi na ulazaji bomba zenye urefu wa mita 32,545,kujenga vioski vya kuchotea maji 15.

Alisema,kazi nyingine zinazopaswa kufanyika ni kusambaza huduma ya maji katika taasisi 7,kununua mashine ya kusukuma maji,kuunganisha umeme katika chanzo,kujenga chemba na kuweka alama kwenye njia kuuza bomba.

Mkazi wa kijiji cha Chitoholi Somoe Mshamu alisema,awali walikuwa wanapata maji kwenye vyanzo vya asili na milima inayozunguka kijiji hicho ambako changamoto kubwa iliyokuwepo kutumia muda mrefu na kukutana na wanyama wakali wakiwemo Simba, Fisi na Nyoka.

Ameishukuru Serikali kwa kuwajengea mradi huo ambao umekuwa mkombozi katika maisha yao,kwani hawatatumia muda mrefu kwenda kutafuta maji badala yake watajikita kufanya shughuli zao za maendeleo.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Hadija Kazumali alisema,kwa muda mrefu walikuwa kwenye mateso kwa kutumia maji ya mito ambayo maji yake hayakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments