Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida NUSRAT HANJE amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa kupeleka huduma katika maeneo yao.
HANJE alisema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kata ya Makiungu, akifunga Bonanza la michezo la "Hanje Mashabiki Bonanza" ulioshirikisha michezo mbalimbali.
Alisema kutokana na juhudi hizo anazozifanya na serikali yake kutatua changamoto, Wananchi waendelee kumuunga mkono ili Nchi ipige hatua za maendeleo katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii.
HANJE alisema serikali inatekeleza miradi mingi ya maendeleo nchi nzima inayosaidia kupunguza au kuziondoa kabisa changamoto zinazowakabili wananchi.
Katika hatua nyingine NUSRAT HANJE aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Alisema watu wote wenye sifa za kupiga Kura na kugombea nafasi mbalimbali wajitokeze kugombea ili wapate nafasi ya kuingia katika ngazi za maamuzi kwenye serikali za Vijiji.
Aidha alitoa wito kwa vijana na wanawake kujitokeza katika Uchaguzi huo wa serikali za mitaa kwani vijana na wanawake wanauwezo kuongoza endapo wakipatiwa nafasi za kuongoza.
Aliwataka vijana pia kuendelea kuilinda amani iliyopo na waache kuwafuta watu wanaotaka kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini.
Hata hivyo katika suala la Ukatili wa Kijinsia, HANJE aliwataka wananchi kupinga vitendo vya Ukatili wa Kijinsia unaofanywa katika Jamii.
Alisema kuna baadhi ya watu bado wanafanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto jambo ambalo halikubaliki katika Jamii.
Hata hivyo katika suala hilo, aliwataka Wanaume wanaofanyiwa vitendo vya Ukatili wa Kijinsia kuacha kuogopa kusema ili waweze kusaidiwa.
HANJE alisema kuna baadhi ya Wanaume wanaofanyiwa vitendo hivyo vya Ukatili wa Kijinsia na wake zao, lakini wanaendelea kuficha na kuumia kwa kuogopa kuchekwa na Jamii zinazowazunguka.
Bonanza hilo la Hanje Mashabiki Bonanza lilishirikisha michezo mbalimbali ikiwemo Mipira wa Miguu, Mpira wa Petee, Kukimbia na Magunia, kufukuza Kuku, kukimbia na Mayai, shindano la kunywa Soda na Drafti, ambapo zawadi mbalimbali zilitolewa kwa washindi wa michezo hiyo.
0 Comments