KAMPENI KUINUA VIJANA KUZINDULIWA JULAI 6, 2024 DAR

 


Na Mwandishi Wetu
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umewataka vijana na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa Kampeni maalumu ya vijana itakayo jadili fursa zilizopo kwa vijana katika jamii.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 04, 2024 Jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa UVCCM Jokate Mwegelo amesema kampeni hiyo itazinduliwa siku ya Julai 6, katika Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es salaam.

Jokate amesema uzinduzi wa kampeni hiyo utaongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi huku Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Mohammed Ali Kawaida na Wenyekiti wa Chama na Jumuiya kutoka katika mikoa mbalimbali nchini watashiriki kikamilifu katika uzinduzi wa kampeni hiyo.

"UVCCM inawaalika Watanzania wote hususani vijana kujitokeza kwa wingi katika siku hii ya uzinduzi wa kampeni hii na kushiriki kikamilifu na kwa ufanisi wa hali ya juu katika kampeni hii mara baada ya uzinduzi wake kwasababu sisi ndio Tanzania ya sasa na ya baadaye.

"Niwahakikishe vijana wote kwamba, CCM inatambua kuwa vijana tunayo nguvu kubwa sana ya kuibua mawazo mapya, kuleta ubunifu na upekee katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi yetu," amesema Jokate.

Ameongeza kuwa, CCM ilianzishwa kwa dhumuni la kuleta mageuzi na maendeleo makubwa ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni kwa nchi yetu, ambapo tangu kuanzishwa kwake vijana wamekuwa mstari wa mbele na wameaminiwa kushika hatamu katika majukumu mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa maono ya Chama Cha Mapinduzi yanatimia.

Pia Jokate amesema siku hiyo itakuwa fursa kwa vijana kuhamashishwa kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura pamoja na kuwahamasisha vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

"Kampeni hii itaambatana na kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa hususani kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura pamoja na kugombea katika nafasi za uongozi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu," amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments