MRADI WA UJENZI WA MABWENI NA MADARASA NIT KUKAMILIKA OKTOBA MWAKA HUU

 

NAIBU Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile, ameutaka uongozi wa Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) kuhakikisha mradi wa ujenzi wa majengo ya mabweni na madarasa ya wanafunzi unakamilika kwa wakati ili wanafunzi waweze kutumia majengo hayo.

Ameyasema hayo leo Julai 22,2024 Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya ukaguzi kujionea maendeleo ya ujenzi huo katika Chuo Cha NIT ambapo ameridhishwa na kasi ya ujenzi na kuwataka wakandarasi kuendelea na kasi zaidi ili kukamilisha ujenzi kwa wakati.

Aidha Naibu Waziri amemuagiza Mkuu wa Chuo hicho Cha Usafirishaji kuhakikisha anasimamia majengo hayo ili yajengwe kwa ubora unaotakiwa na kukamilika kwa wakati.

Amesema majengo hayo wanatarajia yatakamilika mwezi Oktoba mwaka huu kabla ya muhula mpya wa masomo kuanza ambapo wanafunzi waliokosa nafasi katika mabweni ya chuo nao waweze kunufaika kupata nafasi katika majengo hayo.

Pamoja na hayo, Naibu Waziri ameutaka uongozi wa Chuo kuzalisha wataalamu wa kutosha kwajili ya kusaidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ili kuondokana na uhaba wa wataalamu wenye ujuzi katika sekta ya uchukuzi.

"NIT tunawategemea na kuwatumainia nyie ndio mtatusaidia kuzalisha wataalamu,sio miradi imekamilika tunategemea wataalamu kutoka nje wakati chuo chetu kipo na kinauwezo wa kuzalisha wataalamu na wenye uwezo kwenye sekta ya uchukuzi" amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi wa EASTRIP ambao unafadhili ujenzi wa majengo matano chuoni hapo ambapo majengo mawili ni kwa ajili ya bweni ambayo yanayobeba watu 752

Amesema majengo matatu kati ya matano yanayojengwa chuoni hapo ni kwa ajili ya madarasa pamoja na maabara ya wanafunzi wa masomo ya anga, wahandisi pamoja na wahudumu."Tanzania kwa sasa hatuna chuo cha serikali kinachotoa mafunzo ya urubani, serikali imetununulia ndege mbili tunatarajia kuanza mafunzo haya kabla ya mwisho wa mwaka huu"amesema

Ujenzi huo ni jumla ya majengo matano ambapo majengo mawili ni kwa ajili ya mabweni yanayotarajiwa kubeba watu zaidi 1500 na majengo matatu ni majengo kwa ajili ya madarasa na maabara ya wanafunzi wa anga.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments