Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko amebabidhi kompyuta tano zilizotolewa na kampuni ya Tumbaku ya Alliance One, kwenda kwa vyama vya msingi vya Wakukuna wa Tumbaku vilivyofanya vizuri kwenye msimu wa zao hilo mwaka huu.
Zawadi hizo zenye thamani ya shilingi milioni 26 zimekabidhiwa kwa vyama vya msingi, baada ya kuibuka washindi kati ya vyama 115 ambavyo vina mikataba na kampuni hiyo nchini.
Makabidhiano hayo yamefanyika mwisho mwa wiki kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani ambayo kitaifa yamefanyika kwenye viwanja vya Nanenane, mkoani Tabora.
Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti, amesema zawadi hizo ni motisha kwa vyama vya msingi vya Wakulima wa Tumbaku vilivyofanya vizuri kwenye msimu wa tumbaku wa 2023/2024, baada ya kuvishindanisha kwa vigezo mbalimbali.
Amevitaja vigezo vya ushindi huo ni kufanya malipo kwa wanachama wao kwa wakati, kufikia au kuvuka malengo ya makisio ya uzalishaji wa zao pamoja na utunzaji bora wa kumbukumbu ya mahesabu ya chama husika.
“Tunavishindanisha vyama hivi vya msingi almaarufu Amcos kwa lengo la kuvisaidia kubadilisha mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu kutoka kwenye makaratasi ili kwenda kuwa kidigitali zaidi,” amesema.
Amesema mpango huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka jana, ambapo pia zilitolewa kompyuta kama hizo tano, utasaidia kupunguza kama siyo kuondosha kabisa upotevu wa nyaraka muhimu za vyama hivyo.
Viongozi wa vyama hivyo wakipokea zawadi hizo kwa niaba ya vyama vyao, wameishuru kampuni hiyo kwa mpango wao huo na kuahidi kuendelea kufanya vizuri zaidi siku zijazo.
Vyama vilivyopata kompyuta hizo ni Ilolangulu Amcos cha wilaya ya Uyui, Igwisi Amcos cha wilaya ya Kaliua na Unyanyembe Amcos cha wilayani Sikonge, vyote hivi vya mkoa wa Tabora.
Vingine ni Kikubhagulu Amcos cha wilayani Uvinza mkoani Kigoma na kingine ni Tembo Amcos cha Ushetu, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Mwenyekiti wa Kikubhagulu Amcos Kudra Diyusa ameishukuru kampuni hiyo kwa kuzawadiwa baada ya kufanya vizuri katika wilaya yao ya uvinza.
“Sisi chama chetu msimu huu tulipewa makisio ya tani 155 na badala yake tumevuka lengo kwa kuvuna tani 220, ambazo tumeuza zote na mpaka sasa tumelipana wote kwa asilimia mia moja,”amesema.
Naye Katibu Menaja wa Tembo Amcos Alphonce Simon ameishukuru kampuni hiyo kwa zawadi ya kompyuta mpakato kwani ni ishara ya kutambua kazi nzuri waliyoifanya.
“Kampuni ya Alliance One walitupatia makisio ya kilo 350,000 sawa na tani 350, na kwa kweli tumefanikiwa kufikia makisio hayo kwa asilimia mia moja na mpaka sasa tumefanya malipo yote kwa wanachama wetu,” amesema.
Wakati huo huo kwenye sherehe ya ufungaji wa maadhimisho ya ushirika, Naibu Waziri Mkuu amepongeza wanunuzi wa zao la tumbaku, huku akiwataka kuongeza kasi ya misaada yake kwa jamii ili kwamba wakulima waaweze kuwa sehemu ya mafanikio yanayotokana na zao hilo.
“Nimeambiwa kwamba msimu huu pekee manunuzi ya tumbaku yalifikia dola za kimarekani milioni 300 sasa tunawaombeni sehemu ndogo tu ya kiasi hicho iende kwenye misaada ya jamii na kwa kweli itapendeza sana,” alisema.
Hata hivyo Wakili Magoti amesema kampuni ya Alliance One inatoa jumla milioni 400 kila mwaka kama misaada ya jamii ambapo misaada hiyo inatolewa kwenye mazingira,afya na elimu.
Naibu Waziri pia amewaasa wakulima wa tumbaku nchini kuanza utaratibu wa kukatia bima mazao yao ili kwanza waweze kupata fidia pale wanapofikwa na majanga kama vile ya elnino ambayo yamewakumba msimu huu.
Naye Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema serikali imeamua kutoa fidia ya shilingi bilioni 13 kwa wakulima mbalimbali wa tumbaku ambao mazao yao yaliathiriwa na mvua za elnino msimu wa mwaka 2023/24.
Amesema pesa hizo zitapelekwa moja moja kwa wakulima kwenye akaunti zao baada ya vyama vya ushirika kuwasilisha majina ya wakulima hao kwenye vyombo vya fedha.
Aidha amesema kuanzia mwaka huu, serikali itaanza kutoa ruzuku kwa wakulima wa zao tumbaku ambapo serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 13.3 kwa ajili ya kununulia mbolea ya zao hilo kwenye msimu wa mwaka 2024/2025, ambazo alisisitiza kuwa pesa hizo zitaenda moja kwa moja kwenye shirika la mbolea nchini TFC.
Kuhusu uzalishaji wa zao hilo amesema sekta ndogo ya tumbaku imezidi kukua na kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo mwaka 2022/21 jumla ya tani 60,000 zilizalishwa, wakati mwaka 2022/23 jumla ya tani 120,000 zilizalishwa.
“Makadirio ya uzalishaji kwa mwaka 2023/24 yalikuwa tani 170,000 lakini kwa kuwa kulikuwa na majanga ya elnino, hatukuweza kufikia lengo hilo kwa asilimia 30, hata hivyo nawashukuru wanunuzi kwa kuweka madaraja ya bei kuwa mazuri lengo likiwa ni kufidia wakulima kwani tumbaku ilinunuliwa kwa wastani wa dola mbili,”alisema.
Ametoa maagizo kwamba kuanzia sasa mikataba ya kilimo kati ya wanunuzi na wakulima itakuwa ya miaka mitatu badala ya mwaka mmoja, huku kila mwaka wawili hao wakijadiliana kuhusu bei ya mwaka mmoja hadi mwingine.
Waziri Bashe ameyashauri mabenki ambayo yaliwakopesha wakulima wa tumbaku na ambao wamepata hasara kwenye majanga ya mvua za El Nino kuwasiliana na wakulima hao ili wabadilishe mpango wa ulipaji mikopo hiyo kwa kipindi kirefu zaidi, badala kuwabana zaidi,lengo likiwa kuendeleza zao hilo.
Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko(wa pili kushoto) akipokea moja kati ya kompyuta mpakato tano
kutoka kwa Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya Alliance One David Mayunga, ikiwa ni msaada wa kampuni hiyo kwa vyama vya msingi bora vya tumbaku vinavyofanya kazi na kampuni hiyo.Wengine pichani ni Waziri wa Kilimo Hussein Bashe(kushoto),Mwenyekiti wa Shirikisho la Ushirika nchini TFC Charles Gishuli(katikati),Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambaye pia ni Mkurugenzi Mtedaji wa CRD, Abdulmajid Nsekela(wa pili kulia) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Said Mkumba(kulia).
Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko(wa pili kushoto) akikambidhi kompyuta mpakato
Rashid Sikwala, ambaye ni Katibu Meneja wa Muloku Amcos kilichopo huko Ilolangulu wilayani Uyui, mkoani Tabora region,ikiwa ni sehemu ya msaada wa laptop tano uliotolewa na kampuni ya tumbaku ya Alliance One kwa vyama bora vinavyofanya kazi na kampuni hiyo.Wengine pichani ni Waziri wa Kilimo Hussein Bashe(kushoto),Mwenyekiti wa Shirikisho la Ushirika nchini TFC Charles Gishuli(katikati),Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambaye pia ni Mkurugenzi Mtedaji wa CRD, Abdulmajid Nsekela(wa pili kulia) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Said Mkumba(kulia).
0 Comments