Imeelezwa kwamba Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni za Ununuzi wa Umma ya mwaka 2024 itarahisisha mchakato wa ununuzi kwa watumiaji wa Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma wa Kielekroniki (NeST), nchini.
Hayo yameelezwa leo tarehe 17 Julai, 2024 na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Sheria mpya ya Ununuzi na Kanuni za Ununuzi wa Umma kwa Menejimenti, Bodi ya Zabuni, Maafisa Ununuzi na Maafisa Sheria kutoka Ofisi za TARURA Makao Makuu na ofisi za TARURA Mkoa wa Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Jiji, Mtumba, jijini Dodoma.
Mhandisi Seff amesema kwamba mafunzo hayo ni muhimu sana kwani yanalenga kuondoa kero na malalamiko ya mara kwa mara kwa watumiaji pamoja na watoa huduma.
“Mafunzo ya mabadiliko ya sheria ni muhimu sana kwenu na yanaenda kujenga uwezo katika kutekeleza majukumu ya kila siku kwenye upande wa Ununuzi”.
“Niwasihi, kutumia mafunzo haya kujadili changamoto ambazo mlikua mnakutana nazo kwenye utelekezaji wa majukumu yenu ili kuweza kupata suluhisho kwa yale ambayo yapo ndani ya uwezo wetu, na yale ambayo yatahitaji PPRA tutafanya utaratibu wa kuyawasilisha”.
Aliongeza kusema kwamba eneo la ununuzi huwa linalalamikiwa sana hivyo Serikali imesikia kilio na kutoa jibu kwa kuleta Sheria mpya iliyoanza kutumika Juni, 2024 na kanuni mpya zilizoanza kutumika Julai, 2024.
Hata hivyo Mtendaji Mkuu huyo amesema wakiwa katika utekelezaji wa kazi kwa mwaka wa fedha 2024/25 wameona ni vyema kuwafanyia mafunzo watumishi hao ili wapate uelewa na kufahamu mabadiliko yaliyofanyika kwenye Sheria na Kanuni zake.
0 Comments