WAZIRI MKUU: WATANZANIA LIMENI MAPARACHICHI

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wana-Iringa na Watanzania kwa ujumla waingie kwenye kilimo cha Parachichi kwa kuwa zao hilo linachochea ukuaji wa uchumi. 

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali ilikuwa ikitafuta masoko kwa ajili ya maparachichi yanayozalishwa nchini badala ya kutegemea nchi jirani pekee.  “Tumeshapata soko la moja kwa moja kwa ajili ya maparachichi yetu nchini China na India na tumegundua ya kwetu yana thamani kubwa na ubora wa hali ya juu ukilinganisha na maparachichi kutoka nchi nyingine.”

Ametoa wito huo jana jioni (Jumapili, Julai 7, 2024) wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali mara baada ya kukagua mradi wa kitalu cha miche bora ya parachichi unaomilikiwa na kikundi cha vijana cha Chilongola, kilichopo kata ya Upendo, Mafinga Mjini, mkoani Iringa.

Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania waingie kwenye mpango wa kuzalisha miche ya zao hilo ili kuongeza idadi ya uzalishaji wa maparachichi. “Maparachichi yetu yana ubora mkubwa. Na hii ni baada ya kupima udongo nchini kote na kubaini kuwa tuna maeneo yenye udongo unaofaa kwa kilimo hiki,” amesema.

Akizungumzia suala la barabara kama lilivyowasilishwa na wana kikundi hao, Waziri Mkuu amesema miundombinu ya barabara za kwenda mashambani linaratibiwa vizuri na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).


Kuhusu suala la kukosa mlango wa malimbichi bandarini, Waziri Mkuu Majaliwa amesema analipokea suala hilo na kuahidi kuwa atalifuatilia.


Mapema, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema Serikali imeshasaini mkataba na kampuni ya Afac Engineering ambayo itajenga kiwanda cha kusindika maparachichi katika eneo la Nyololo ambapo katika awamu ya kwanza, sh. bilioni 3.4 zitatumika.


“Wana-Mufindi ni watu wanaolima sana. Mbunge wenu amesimamia ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan ya kujenga kiwanda cha kusindika maparachichi. Mkataba ulisainiwa na kabla ya Ijumaa ijayo, tutamkabidhi eneo mkandarasi ili aanze kazi,” alisema.


Akielezea kuhusu kusuasua kwa zao la chai, Naibu Waziri huyo alisema kuwa Serikali inatambua changamoto iliyokuwepo ya kiwanda cha DL lakini tayari Serikali imeshafanya maamuzi ya kukinunua kiwanda hicho na kukikabidhi kwa wakulima wadogo wadogo wa chai wa Mufindi ili wakiendeshe kupitia ushirika wao.


Kuhusu soko la mahindi, Naibu Waziri Silinde aliwataka wananchi hao wajiandae kuuza mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuanzia Julai 10, mwaka huu na kuahidi kuwa bei itakuwa nzuri. Hata hivyo, hakutaja bei hiyo.


Akifafanua zaidi, alisema: “Kutoka Zambia, tumepokea oda ya tani 650,000 za mahindi. Nchi jirani ya Congo (DRC) nao wametaka tani 500,000 lakini wanataka tuwape tani 200,000 za awali. Kwa hiyo, jiandaeni kuuza mahindi kuanzia tarehe 10 Julai, 2024.”


Naye, Mkurugeni wa kampuni ya Chilongola Agroforestry & Livestock, Andrew Salika alisema kikundi chao kilianza mwaka 2020 kwa kuzalisha miche 9,000 lakini hivi sasa wana miche 250,000 iliyo tayari kwenda sokoni. “Lengo letu ni kuongeza idadi ya miche bora ambapo mahitaji ni miche 730,000 kwa msimu mmoja,” alisema.


Wakati huohuo, Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi alisema mji wa Mafinga ni miongoni mwa miji iliyopo kwenye mradi mkubwa wa maji wa miji 28 nchini lakini mradi umefikia asilimia 18 tu kutokana na kusuasua kwa kasi ya mkandarasi.


Aliiomba Serikali isimamie kwa karibu ujenzi wa barabara ya Mafinga hadi Mgololo kwa kuwa wilaya ya Mufindi inabeba uchumi wa mkoa mzima wa Iringa. “Barabara hii ikiisha, itarahisisha sana usafirishaji wa mazao ya wakulima na kuwa mkombozi wa wananchi wengi,” alisema.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, alimweleza Waziri Mkuu kwamba wilaya hiyo ina ekari 800,000 ambazo ni miti tupu na kati ya hizo, ekari 500,000 ni za miti ya kupandwa. Alisema wilaya hiyo ina viwanda 40 vya kuchakata mazao ya miti pamoja mazao ya kilimo kama chai na pareto. 

Aliishukuru Serikali kwa kuwapelekea umeme ambapo hadi vijiji vyote 312 vya wilaya hiyo vimepata umeme na kuongeza kuwa hivi sasa wamejipanga kukamilisha uwakaji umeme vitongojini. “Tuna vitongoji 612, ambapo vitongoji 412 vimeshapata umeme na kati ya 200 vilivyobakia, 107 vipo kwenye mpango wa kupatiwa umeme mwaka huu,” alisema.

Waziri Mkuu amefuatana pia na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments