WIZARA YA ARDHI KURASIMISHA MITAA 13 KONDOA MJI

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatarajia kutekeleza mradi wa urasimishaji makazi holela kwenye mitaa 13 ya Mji wa Kondoa mkoa wa Dodoma.

Hayo yamebainishwa tarehe 21 Agosti 2024 na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango katika wilaya Kondoa jijini Dodoma.

Amesema, jumla ya viwanja 11,000 vinatarajiwa kupangwa na kupimwa ambapo ameweka wazi kuwa, kazi hiyo inatekelezwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaofadhiliwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia.

"Kazi hii ya urasimishaji makazi holela katika mji wa Kondoa inatekelezwa kwa fedha za mradi wa LTIP ambazo ni mkopo wa Benki ya Dunia" alisema Mhe. Pinda.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kazi hiyo ya urasimishaji inatarajiwa kugharimu shilingi Bilioni moja na kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2024/2025.

Mhe. Pinda amebainisha kuwa, tayari hatua za awali za utekelezaji kazi hiyo zimeanza kwa kufanyika vikao vya wadau wa sekta ya ardhi ambapo mwenyekiti wake alikuwa mkuu wa wilaya ya Kondoa huku hatua za kumpata mkandarasi zikiwa tayari zimekamilika.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda yuko kwenye ziara ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango katika mkoa wa Dodoma ambapo Makamu wa Rais anakagua shughuli za maendeleo kwenye wilaya za mkoa huo. Tayari Makamu wa Rais ameshatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya za Chamwino, Mpwapwa, Kongwa, Kodoa na Chemba.

Naibu Wzairi wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wilayani Kondoa wakati wa ziara ya Mkamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango tarehe 21 Agosti 2024.


Sehemu ya wananchi wa kondoa waliojitokeza katika ziara ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango katika mkoa wa Dodoma.

Naibu Wzairi wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akinyanyua mikono kwenye mkutano wa hadhara wa Mkamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango katika ziara yake wilayani Kondoa tarehe 21 Agosti 2024. Kulia ni Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Methew Kundo.
Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango akisalimiana na viongozi mara baada ya kuwasili kwenye shule ya wanafunzi wenye uhitaji maalum Iboni wllayani Kondoa tarehe 21 Agosti 2024 (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments