POLISI YAKEMEA JAMII KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI

 

JESHI la polisi limekemea matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi Mkoani Manyara kwa matukio ya magari kuchomwa moto na watu kujeruhi kwa kisingizio cha wizi wa watoto.


Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na msemaji wa jeshi la polisi Tanzania, David Misime, matukio matatu kama hayo yamejitokeza mkoani Manyara.

Misime amesema hivi karibuni kumejitokeza tabia ambayo si nzuri ambapo watanzania wasipoelimishana na kukemea wengi watajeruhiwa, kuuawa na hata kuharibiwa mali zao kwa kisingizio cha wezi wa watoto.

Amesema matukio hayo yameshawatokea baadhi ya watu walipokuwa safarini kwa usafiri binafsi na kwa bahati mbaya magari yao yakapata hitilafu na moja kuishiwa mafuta.

Ameeleza kuwa matukio matatu kama hayo yameshuhudiwa kwa nyakati tofauti mkoani Manyara kwa watu kujeruhiwa na magari yao kuchomwa moto.

"Tukio la kwanza lilitokea Agosti 14 mwaka 2024 saa 11 jioni katika kijiji cha Bargish wilayani Mbulu ambapo Kurwa Nogu Kabata (38) kibarua wa kutunza miche idara ya Misitu Mbulu alijeruhiwa kwa kushambukiwa na watu waliojichukulia sheria mkononi," amesema Misime.

Amesema Kabata alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili na kusababisha kulazwa hospitali na sasa amehamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi chanzo ni tuhuma za uongo kuwa ni mwizi wa watoto.

"Wananchi hao waliojichukulia sheria mkononi kwa kuchoma moto gari namba T 531 DTN mali ya Samson Kabata Madeleka ambapo watuhumiwa saba wamekamatwa kwa kuongoza utendaji wa uhalifu huo.

Ametaja tukio la pili lilitokea Agosti 16 mwaka 2024 saa 3 usiku kijiji cha Sharmo wilayani Babati, ambapo Joshua Bashiru Mussa (34) mchungaji wa Kanisa la Hema la Utukufu akiwa na msaidizi wake walishambuliwa.

Mchungaji Bashiru na msaidizi wake Joseph Charles Athuman (29) mkazi wa Nangara wakiwa wanatoka kwenye mkutano wa injili kijiji cha Oshan wakiwa na gari namba T 360 AJH aina ya Toyota Corolla waliishiwa mafuta.

"Wakiwa na na gari katika kijiji cha Sharmo walishambuliwa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi kisha kuchoma moto gari kwa tuhuma kuwa ni wezi wa watoto na watuhumiwa tisa wa tukio hilo tunawashikilia," amesema.

Amesema tukio la tatu la watu kushambuliwa lilitokea Agosti 25 mwaka 2024 saa 11 jioni katika kijiji cha Maghgang wilayani Mbulu, ambapo Anthony Francis (44) dereva na Anorld John (37) mpishi na Mina Sekobaha (36) muuguzi wote wakazi wa jijini Arusha.

Amesema watu hao wakiwa na gari aina ya Toyota Raum yenye namba T 118 DHZ walishambuliwa na kujeruhiwa seheju mbalimbali za mwili na watu waliojichukulia sheria mkononi na kulichoma moto gari hilo.

Amesema tukio hilo lilitokea baada ya gari hilo kupata pancha wakati wakitokea kwenye sherehe ya harusi ya ndugu yao iliyofanyika kijiji cha Kidarafa wilayani Mkalama mkoani Singid ambapo watuhumiwa 10 wamekamatwa kwenye tukio hilo.

"Francis baada ya matibabu ya awali, amehamishiwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC iliyopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kutokana na kujeruhiwa kwenye taya na maeneo mengine ya mwili," amesema Misime

Ametoa wito kwa wananchi kuachana na vitendo hivyo na ushabiki wa kuhamasisha uhalifu kwenye mitandao ya kijamii kwani uhalifu kama huo usipokemewa ukaachwa unaweza kumpata yeyote katika safari za hapa na pale au katika matembezi ya kawaida.

"Kinachotakiwa kufanyika kama mnawatilia watu shaka ni kutoa taarifa kwa uongozi wa eneo husika au, polisi na siyo kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume na sheria za nchi," amesema Misime.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments