Wabadhirifu mikopo ya halmashauri kukiona

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema hatosita kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria maofisa maendeleo ya jamii, wasimamizi wa fedha, waratibu wa mikopo, wahasibu na maofisa Tehama wa mikoa na wilaya watakaojihusisha na ubadhirifu wa fedha za mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wanye ulemavu.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, wakati akifunga mafunzo ya wasimamizi wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambayo inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri zote nchini.

“Mikopo hii inatolewa na serikali kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi wanaweke, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujikomboa kiuchumi kwa kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali, hivyo sitosita kuwachukulia hatua watakaokwamisha makundi lengwa kupata mikopo,” Mchengerwa amesema.

SOMA: Mikopo 10% yaiva, mfumo, kanuni tayari

Mchengerwa amesema mikopo hiyo ikisimamiwa vizuri na kuwafikia walengwa itabadilisha maisha ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hivyo amewataka washiriki wa mafunzo hayo waende kutoa elimu ya namna bora ya kuitumia mikopo hiyo kuboresha maisha yao ili waweze kufanya marejesho kwa wakati na kuwezesha wengine kunufaika.

Amewataka wasimamizi wa mikopo ya asilimia 10 kuratibu utoaji wa mikopo hiyo kwa uzalendo ili iwanufaishe walengwa na iwe na tija kwa jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla kama ilivyo kusudiwa na Serikali.

SOMA: ‘Maombi mikopo ya halmashauri sasa kidijitali’

Kufikia mwaka wa fedha 2024/25  fedha ambazo zimetengwa kutoka kwenye marejesho ya mikopo ya nyuma pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri tangu utoaji wa mikopo hii ulipositishwa ni zaidi ya Sh bilioni 160 kwa halmashauri zote nchini.

Ikumbukwe kuwa mikopo hii inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri zote nchini.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments