VETA Yasaini Makubaliano na Henan Polytechnic Institute Kuendeleza Elimu ya Ufundi Stadi katika Kilimo na TEHAMA

 Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano na taasisi ya Henan Polytechnic Institute, kutoka Nanyang, China ili kushirikiana kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika nyanja za kilimo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, (TEHAMA).

Makubaliano hayo yamesainiwa jana, tarehe 11 Novemba 2024, katika Chuo cha VETA Kihonda.

Katika makubaliano hayo chuo cha VETA Kihonda kitanufaika katika nyanja ya kilimo na Chuo cha VETA Kipawa kitanufaika katika sekta ya TEHAMA.

Aidha, walimu na wanafunzi kutoka vyuo vya VETA Kihonda na Kipawa watajengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo katika maeneo ya Kilimo na TEHAMA ili kuboresha elimu na mafunzo ya ufundi stadi na kuhakikisha wanazalisha wahitimu bora wenye kukidhi ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya Tanzania.

Katika mpango huo, walimu na wanafunzi kutoka pande zote mbili watapata fursa za kutembeleana na kubadilishana uzoefu baina yao ili kuhakikisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanatolewa katika ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.

Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, ameishukukuru taasisi ya Henan Polytechnic kutoka China kwa kuona VETA ndio sehemu sahihi ya kuleta teknolojia mpya katika masuala ya kilimo na TEHAMA.

CPA. Kasore amesema kupitia makubaliano hayo, VETA inatarajia kunufaika kwa kiasi kikubwa, hasa katika kupata utaalam mpya ambao utawezesha vijana wa kitanzania kupata elimu na mafunzo ya ufundi stadi bora na yenye viwango vya kimataifa ambayo yatakidhi ushindani katika soko la ajira.

“Ninaamini, kupitia ushirikiano huu, ndoto ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha vijana wa kitanzania wanapata elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujikwamua kimaisha inaenda kutimia, naomba ushirikiano huu uwe chachu katika kuzalisha vijana ambao wataweza kushindana katika soko la ajira kimataifa katika kujenga uchumi wao na taifa la Tanzania,” CPA. Kasore ameongeza

Amesema, atapenda kuona mahusiano hayo yanakuwa ya kudumu na kuleta manufaa makubwa baina ya nchi zote mbili, na kwa upande wa VETA, inatarajia kupata wataalamu waliobobea katika maeneo yaliyoainishwa ili kuzalisha vijana wenye weledi mkubwa na ufanisi katika elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments