Tanzania ni mfano miaka 63 ya Uhuru


Miaka zaidi ya 60 sasa tangu Waafrika wapate Uhuru, tumeshuhudia katika mataifa mengi ya Bara hili wanasiasa wakigombea madaraka na kufikia kuhatarisha amani ya nchi husika kwa sababu ya kutaka uongozi.

Ufike wakati sasa Umoja wa Afrika (AU) uweke masharti magumu kwa wanasiasa wanaosababisha machafuko na kuvurugika kwa amani na utulivu kutengwa kabisa katika umoja huo.

Leo Desemba 9, 2024, imetimia miaka 63 tangu Tanganyika ipate uhuru wake mwaka 1961, kisha Aprili 26, 1964 Tanganyika ikaungana na Zanzibar na kuunda taifa la Tanzania.

Watanzania tunafurahia matunda ya uhuru, lakini wapo wenzetu wanaendelea kuteseka licha ya kupata Uhuru. Miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika uwe mfano kwa wengine Afrika.

Naamini mataifa ya Afrika yataendelea kujifunza nini Watanzania wanakifanya, viongozi wanaachiana madaraka kwa amani, wananchi wanaishi kwa amani na kila mmoja anafanya shughuli zake.

Machafuko katika baadhi ya nchi yananifanya kumkumbuka, muimbaji mahiri wa muziki wa taarab kutoka Barawa, Somalia, Asha Abdow Suleiman, maarufu kwa jina la Malika ameimba: “Hii ni ajabu gani Manahodha baharini kugombania sukani.”

Sehemu ya wimbo huo unaimbwa: “Nguo wamezipania, manahodha wazivuta, sukani ishalegea na tanga washalikata, lakini wagombania hawataki kuiacha, Hii ni ajabu gani ilozuka duniani manahodha baharini  kugombania sukani…

“Manahodha vita hivyo, baharini wajigamba, sukani wateteavyo mawimbi yashawakumba na hivi chombo chendavyo sasa kitapanda mwamba.

 

Hii ni ajabu gani ilozuka duniani manahodha baharini kugombania sukani?

“Mimi naiacha bahari, siviwezi vita vyao, na kila  nikifikiri nauona mwisho wao utakuwa misumari ni mbalimbali na mbao.”

Wimbo huo wa Malika umesheheni salaam nzito na za wakati. Inafaa sana kuwakumbusha wanasiasa kuacha kugombea sukani baharini, kwani kwa namna hali inavyokwenda, chombo kitapanda mwamba na misumari itakuwa mbalimbali na mbao hali itakayosababisha maafa kwa jamii.

Nami nauliza hii ni ajabu gani ilozuka hapa duniani kwa Bara la Afrika kila kukicha machafuko yanayosababishwa na kutaka madaraka?

Afrika haumalizi mwaka bila kusikia kituko cha kisiasa, waasi, machafuko au mkasa wowote wa kisiasa unaosababisha watu wachache kunyakua madaraka ya dola kwa nguvu!

Afrika tangu kwa miongo mingi imekumbwa na mizozo ya kisiasa,kijamii na kwa sehemu kubwa mizozo hiyo ndio chanzo cha kudumaa kwa maendeleo ya Bara la Afrika kiuchumi.

Nchi nyingi mara baada ya uhuru zikajikuta zinatumbukia katika migogoro ya kuwania madaraka,wengine waliposhindwa kwenya uchaguzi waliamua kukimbilia msituni kuanzisha vita.

MWENGE WA UHURU

Baadhi ya migogoro inatia aibu,wapo watu wamekuwa waking’ang’ania madaraka, wengine ni kama vile wao ndio wenye uwezo hakuna mtu mwingine ambaye anaweza kutawala.

Matokeo ya imani hiyo ndio kuzuka kwa malalamiko na machafuko ambayo yanasababisha madhara makubwa kwa jamii husika.

Matukio ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Afrika ni pigo kwa ustawi wa demokrasia na ukuaji wa uchumi.

Sifa ya Taifa dhaifu ni kuzuka kwa mapigano ya kikabila, ya kieneo na pia serikali husika kupoteza udhibiti wa eneo katika nchi.

Waafrika tuna kila sababu ya kukataa migogoro ya kivita,watu watumie njia za kisiasa katika kushawishi wananchi kuwaunga mkono,lakini si kutumia njia za kivita katika kufikia malengo. 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments