Majaliwa: Tanzania itakuza biashara na EU

 

SERIKALI ya Tanzania imesema itaendelea kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na nchi za Umoja wa Ulaya (EU).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu ya Magogoni, Dar es Salaam jana alipozungumza na Balozi wa EU nchini, Christine Grau.

“Inatia faraja sana kuona kuna ukuaji wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya, Umoja wa Ulaya umewekeza takribani Euro bilioni tatu nchini, hii kwa kiasi kikubwa imechangia kutengeneza ajira na makusanyo ya kodi,” alisema Majaliwa.

Alisema Tanzania itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kuzivutia sekta binafsi kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Majaliwa alisema Tanzania inathamini msaada unaotolewa na EU kuchangia shughuli za maendeleo nchini.

“Katika kipindi cha 2021-2027, Umoja wa Ulaya umetenga Euro milioni 703 ili kusaidia mipango ya maendeleo nchini Tanzania, tunakushukuru hasa kwa kujitolea kwenu kuimarisha ushirikiano huu,” alisema.

Awali, Majaliwa alikutana na Balozi wa Jamhuri ya Korea, Ahn-Eun-Ju akamweleza Tanzania inajivunia ushirikiano na nchi hiyo kwenye sekta mbalimbali za maendeleo.

“Tanzania na Jamhuri ya Korea zinaushirikiano mkubwa wa kibiashara kwa miaka mingi, mnamo mwaka 2023, kiwango cha ufanyaji biashara kilifikia Dola milioni 672.7, ikilinganishwa na Dola milioni 280.4 mwaka 2022,” alisema.

Aliongeza: “Tunatambua kuwa kampuni za Jamhuri ya Korea zimewekeza katika sekta mbalimbali nchini Tanzania, kama viwanda, usafirishaji na ujenzi, hivyo kuchangia maendeleo ya nchi zetu. Tunathamini uwekezaji huu”.

Aidha, Majaliwa alimweleza balozi huyo aone namna ya kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata nafasi za kazi nchini Korea hasa kwenye sekta ya uzalishaji.

“Kwa upande wetu sisi tutahakikisha Watanzania wanakuwa na vigezo stahiki vinavyohitajika ili waweze kufanya kazi,” alisema.

Balozi Ju alimweleza Majaliwa kuwa katika kipindi chote atakachokuwa balozi nchini atasimamia na kuendeleza masuala ya uwekezaji kwa faida ya nchi zote mbili.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments