KIGOMA – Timu ya soka ya Kajuna FC kutoka mkoani Kigoma imeendelea kutamba kwenye mashindano ya Mabingwa wa Mikoa, baada ya kushinda mchezo wake wa tatu mfululizo katika kundi B kwenye kituo cha Kigoma.
Katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Lake Tanganyika, Kajuna FC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Magic Pressure kutoka Singida, ushindi uliowafanya kufikisha pointi 9 na kuongoza kundi hilo lenye jumla ya timu saba.
Mshambuliaji Ally Sonso alikuwa shujaa wa Kajuna FC baada ya kufunga mabao yote mawili katika kipindi cha pili, huku Ramadhan Ramadhan akifunga bao la kufutia machozi kwa Magic Pressure. Mchezo huo ulisimamiwa na mwamuzi Ndaki Mussa kutoka Tanga.
Kajuna FC sasa imeshacheza michezo mitatu kati ya sita inayopaswa kuchezwa kwenye kundi hilo, na nafasi yao ya kufuzu robo fainali inaonekana kuwa kubwa. Kwa sasa, msimamo wa kundi B ni kama ifuatavyo:
1️⃣ Kajuna FC (Kigoma) - Pointi 9
2️⃣ Home Boys (Katavi) - Pointi 7
3️⃣ Igunga FC (Tabora) - Pointi 4
4️⃣ Kyela FC (Mbeya) - Pointi 3
Ikiwa wataendelea na mwenendo huu, Kajuna FC inatarajia kuwa moja ya timu mbili zitakazofuzu hatua ya robo fainali kutoka kituo cha Kigoma. Mashabiki wa soka mkoani Kigoma wameendelea kuonyesha sapoti kubwa kwa timu yao huku wakiweka matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa wa mikoa.
0 Comments