MAFUNZO YA WALIMU KAZINI KUENDELEA KUTOLEWA

Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya walimu kazIni kwa Walimu wa masomo yote ikiwemo masomo ya Sayansi na hisabati.

Hayo yamebainishwa Machi 28, 2025,  Mkoani Singida na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda wakati akifunga mafunzo ya walimu zaidi ya 890 wa masomo ya Hisabati na Sayansi  yanayotolewa na Wizara kupitia  Mradi wa kuendeleza Elimu ya Sekondari (SEQUIP).

Prof Mkenda amesisitiza kuwa katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 Mwalimu ni kiini katika kufanikisha l lengo la kutoa elimu bora yenye kuwajengea wanafunzi maarifa, kuchagiza fikra tunduizi na ujuzi kwa kizazi cha sasa na baadae .

Amesema kuwa katika ulimwengu wa sasa ambao  Teknolojia inayokua kwa kasi,  masomo ya sayansi na hisabati ni muhimu na hivyo mafunzo ya mbinu za kuyafundisha kwa walimu yatawezesha wanafunzi  kupenda masomo hayo na kufaulu na hivyo taifa kuzalisha wanasayansi watakao chagiza maendeleo.

" Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanakwenda kwa kasi hivyo hatutaki kubaki nyuma, na tuna wajibu wa kuweka misingi bora kwa wanafunzi wetu katika masomo hayo". amesema Mkenda

Ameeleza kuwa katika kuongeza fursa za masomo hayo serikali imechukua hatua mbalimbali  ikiwemo kuongeza shule za sayansi ikiwemo Shule mpya 26 za Wasichana wanaochukua mkondo wa Sayansi lakini pia kuanzisha ufadhili kupitia Samia Scholarship ambao ni asilimia 100 kwa masomo ya Elimu ya Juu kwa wanafunzi wanaofaulu vizuri masomo ya sayansi kidato cha sita. 

Tangu kuanza kwa mafunzo hayo jumla ya Walimu 40,000  wa masomo ya Hesabu na Sayansi kutoka Shule za Serikali wamefikiwa .




TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments