Majaliwa aagiza bidhaa kukidhi viwango

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi za kudhibiti viwango nchini kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa zikiwemo za afya zinakidhi ubora unaotakiwa ili ziweze kushindana katika masoko ya kimataifa.
Ametoa agizo hilo leo Machi 20 baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mitambo ya kuzalisha oksijeni kwa matumizi ya hospitali, ambapo amesisitiza kuwa soko linatakiwa liwe na bidhaa salama, bora, na zinazokubalika kimataifa.
Mitambo hiyo inajengwa katika ofisi za TOL Gases, Temeke Dar es Salaam.
Majaliwa amesema mradi huo utakapokamilika utazalisha lita milioni 4.1 za oksijeni ya matibabu kwa mwaka kuanzia mwaka 2026.
“Hatua hii itaboresha upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na vituo vya afya, pamoja na kupunguza gharama za oksijeni ya matibabu kwa asilimia 35 katika hospitali na vituo vya afya kote nchini, hivyo kuimarisha huduma za afya kwa wananchi,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema mradi huo unaunga mkono juhudi endelevu za Serikali za kuhakikisha oksijeni kwa ajili ya matibabu inapatikana kwa urahisi katika kila kituo cha huduma za afya nchini.
“Mradi huu utaongeza upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na zahanati nchini na kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa ya kupumua ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya akina mama na kuokoa watoto wa Taifa hili,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godfrey Mollel amesema mradi huo ni muhimu kwa sababu oksijeni inayozalishwa kwa njia hiyo inakuwa na viwango vya ubora, hivyo itasaidia kuimarisha huduma za afya zitolewazo nchini pamoja na kupunguza vifo.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases, Daniel Warungu ameipongeza Serikali kwa kujidhatiti katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments