KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Mosses Kusiluka ameziagiza taasisi na mashirika yote ya umma kutumia vizuri huduma wanazotoa kushiriki na kufanikisha uchaguzi mkuu na wasiwe kikwazo.
Aidha, alisema sheria mpya ya Ofisi ya Msajili wa Hazina inatungwa ili kumuwezesha kusimamia vyema majukumu yake na taasisi zilizo chini yake.
Balozi Kusiluka alisema hayo juzi jioni mjini hapa wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.
“Kwa nafasi zenu katika taasisi hizo hakikisheni mnashiriki uchaguzi mkuu ujao na kuufanikisha, kama uko taasisi ya mawasiliano hakikisha mawasiliano yanakuwepo kwa wananchi, kusiwepo na mkwamo katika uchaguzi huo,” alisema Balozi Kusiluka.
Alisema kufanya hivyo kutaufanikisha uchaguzi mkuu ujao ambao taifa linatarajia kuchagua viongozi wake kwa ngazi ya urais, ubunge na udiwani.
Akizungumzia Ofisi ya Msajili wa Hazina, Balozi Kusiluka alisema serikali imefanya uamuzi wa kutunga sheria mpya ya kuongoza ofisi hiyo, ambayo itamwezesha msajili wa hazina kusimamia vyema majukumu yake na taasisi zilizo chini yake.
Alisema hatua hiyo itamfanya msajili aweze kuwajibika vyema na kusimamia taasisi zilizochini yake ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.
Akizungumzia mkutano huo, alisema serikali inategemea kuona tija na ufanisi katika mashirika na kampuni hizo na nyingine ili kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan anayosisitiza kuhusu ufanisi kama kigezo kikuu cha kukuza uchumi.
“Niseme katika hili la mashirika ya umma na kampuni serikali inataka kupunguza ushiriki wake kwa kiwango kikubwa ili kutoa nafasi taasisi na mashirika hayo kuendeshwa kibiashara kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi,” alisema.
Alisema serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji na kwa njia hiyo iko tayari kuuza hisa zake kwa taasisi binafsi za biashara ili jamii ipate wigo mpana kununua hisa na kumiliki hivyo kujiendesha kibiashara.
“Katika hilo lazima tuige mbinu nzuri za kuendesha mashirika yetu,” alisisitiza Balozi Kusiluka.
Katika hatua nyingine, Balozi Kusiluka aliyataka mashirika na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache kuongeza faida ya uwekezaji kutoka asilimia saba ya sasa hadi ifike asilimia 10, mwaka ujao wa fedha.
Alisema hilo linawezekana iwapo watendaji hao wataongeza tija na ufanisi wa utendaji katika kampuni wanazosimamia.
Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 308 ambapo kati ya hizo 56 ni zile serikali ina umiliki wa hisa chache na uwekezaji wa serikali uliofanywa kwao ni wa Sh trilioni 2.9.
Hata hivyo katika taasisi zote 308 zinazosimamiwa na ofisi ya msajili wa hazina Sh trilioni 83.4 zimewekezwa kwenye taasisi ambazo serikali ina umiliki wa asilimia 100 wa hisa.
Akizungumza katika tukio hilo, Balozi Kusiluka aliwapa changamoto watendaji hao kuhakikisha wanaongeza ufanisi wa taasisi zao ili ziweze kuongeza gawio kwa serikali.
Kwa mwaka wa fedha uliopita, serikali ilipata gawio la Sh bilioni 195 kampuni na taasisi zenye zenye umiliki wa hisa chache.
Alisema kuzinduliwa kwa mwongozo ulioboreshwa wa wakurugenzi wa bodi za kampuni na mashirika ambayo serikali ina hisa chache, uliofanywa Machi 26, mwaka huu, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha ni hatua njema ya kuwa na dira.
Awali, Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akizungumza kwenye ufunguzi huo aliwataka wawakilishi wa serikali kwenye bodi za kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Mchechu aliwataka watendaji hao kuzitendea haki nafasi walizopewa ili kuhakikisha kuwa serikali inanufaika na uwekezaji iliofanywa kwenye kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache.
0 Comments