
MAZUNGUMZO ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na waasi wa M23 yanatarajiwa kufanyika leo katika mji mkuu wa Angola. Hii ni kwa mujibu wa ofisi ya rais wa Angola.
Angola imekuwa ikijaribu kuwa mpatanishi kwa lengo kufikia hatua ya kusitisha mapigano la kudumu na kupunguza mvutano kati ya DRC na jirani yake Rwanda, ambayo imekuwa ikituhumiwa kuwaunga mkono M23.
Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, ilitangaza hivi karibuni kwamba itajaribu kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja.
Rais wa Angola, Joao Lourenco aliteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa mpatanishi.
Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita, ilitoa wito wa usitishwaji wa mapigano mashariki mwa DRC kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani leo.

Alitaka mapigano yasitishwe kuanzia saa 6 usiku wa kuamkia Machi 16, 2025 kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani mjini Luanda.
Tunaunga mkono rai ya mpatanishi huyo ya kutaka vitendo vyote vya uhasama dhidi ya raia na azma ya kutwaa maeneo zaidi, visitishwe ili kusaidia kuwapo hali ya utulivu itakayowezesha kuanza kwa mazungumzo ya amani.
Aidha, itakuwa busara kubwa endapo Rais Felix Tshisekedi atakuwa tayari kutii wito huo kwa kukubali ikataa kukaa meza moja na waasi wa M23 ambao serikali yake inawachukulia kama magaidi.
Kwa kila mpenda amani, hususani nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo DRC ni mwenzao, angependa kusikia kama si kuona Rais Tshisekedi akishiriki mazungumzo ya amani yanayolenga kusuluhisha mzozo unaoendelea kati yake na waasi.
Mzozo huu hauna tija kwa ustawi kwa wananchi wa wananchi wa DRC kwani umekuwa na athari kubwa si tu kwa nchi hiyo bali pia kwa ukanda mzima wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Afrika kwa ujumla.
Umesababisha umaskini mkubwa na ukosefu wa huduma muhimu kwa wananchi.

Watu wengi wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa chakula, maji safi na huduma za afya kutokana na mapigano yasiyoisha ambayo yameharibu miundombinu ya kijamii.
Hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi umeendelea kutanda hali inayosababisha uhamaji wa watu na hivyo kuongeza mzigo kwa nchi jirani hususani za EAC.
Wakati mzozo huu unashughulikia masuala ya kisiasa na nguvu za kijeshi, ni muhimu kukumbuka kwamba raia wa kawaida wa DRC wanashuhudia maumivu makubwa na kutengwa na fursa zao za kimaendeleo.
Pande zinazozozana hazina budi kutambua kwamba mzozo huu unaweza kuathiri hata ushirikiano wa kikanda kwani migogoro kama hii inakwamisha juhudi za kushirikiana katika masuala ya kiuchumi na usalama.
Sasa ni wakati muafaka kwa viongozi wa EAC kumsihi na kama si kumshinikiza Rais Tshisekedi kushiriki katika mazungumzo ya amani ikiwa ni pamoja na kushirikisha pande zote na kuweka mbele maslahi ya taifa ili kuleta utulivu na ustawi wa kweli katika EAC.
Ifike wakati ‘wimbo’ huu wa mgogoro kati ya Serikali ya DRC na waasi ufike mwisho na kuondolea EAC na Afrika kwa ujumla doa la kiusalama.
0 Comments